Merkel aikosoa Uturuki kuhusu Syria
21 Machi 2018Kansela Angela Merkel amelihutubia bunge kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani katika muhula wa nne ambapo ameahidi kwamba wimbi la wakimbizi lililoshuhudiwa mwaka 2015 halitojirudia tena.Merkel amekiri katika hotuba yake kwamba mjadala juu ya suala la wahamaiji limeigawa Ujerumani na kulemaza shughuli za nchi hiyo hadi wakati huu.
Kansela Angela Merkel amesema Ujerumani ambayo imefungua milango kuwapokea zaidi ya wahamiaji milioni moja mnamo mwaka 2015 na 2016 inaweza kujivunia hatua hiyo lakini pia akaongeza kusema kwamba hapana shaka pia hatua hiyo ilitokana na hali ya kipekee ya kibinadamu iliyokuweko. Kilichofanyika Ujerumani kwa mujibu wa Merkel ni kuchukua hatua ya kusuluhisha tatizo la kibinadamu kama ilivyopaswa na hali hiyo haipaswi kujirudia.
Amegusia makubaliano ya mwaka 2016 yaliyofikiwa pamoja na Uturuki yaliyonuiwa kuzuia kuwasili kwa wahamiaji pamoja na kukomeshwa kwa shughuli za wanaofanya biashara ya kuingiza watu kwa magendo barani Ulaya, akisema kwamba makubaliano hayo yanakabiliwa na upinzani mkubwa lakini atasimama kila wakati kuyatetea. Hotuba ya Merkel imegusia mambo mbali mbali ikiwemo ya Kimataifa na hapa pia amepata nafasi ya kuzungumza kwa upana zaidi kuhusu hatua ya rais wa Marekani Donald Trump ambapo ameukosoa mpango wa viwango vya kodi ulioanzishwa na rais huyo kuelekea bidhaa za chuma na bati kutoka nje.
Aionya Marekani
Merkel ameionya Marekani kwamba Umoja wa Ulaya uko tayari kuchukua hatua za kulipiza kisasi juu ya sheria hiyo pale itakapobidi, akisema kwamba wanautazama mpango huo wa viwango vya kodi kama mpango usio wa kisheria. Ujerumani inaamini kwamba kujitenga katika suala la ushindani wa kibiashara ni hatua itakayomuumiza hatimaye kila mmoja, na kwa maana hiyo Kansela Merkel amesema Ujerumani na Umoja wa Ulaya wataendelea na mazungumzo pamoja na Marekani kuhusu biashara.
Kansela Merkel ameigeukia pia Uturuki na kuikosoa kuhusu operesheni kubwa ya kijeshi dhidi ya wanamgambo wa kikurdi katika ngome yao ya Afrin nchini Syria akisema ni jambo lisilokubalika kwa kuangalia kinachotokea Afrin ambako maelfu kwa maelfu ya raia wanaouwawa.
"Nniseme katika muktadha huu,kwamba pamoja na maslahi ya kiusalama ya Uturuki ni jambo lisilokubalika kwa kile ambacho kinaendelea Afrin ambako maelfu kwa maelfu ya raia wanateswa, kuuwawa na kulazimika kukimbia makaazi yao. Tunalaani kwa nguvu zote hatua hiyo.''
Anaamini kiongozi huyo wa Ujerumani kwamba mgogoro wa Syria unahitaji suluhisho la kisiasa sambamba na hatua za kibinadamu za kuwasaidia raia ambapo katika hilo ameonya kwamba mashambulizi yanayoendelea kwa hivi sasa katika nchi hiyo yanaongeza tu hali ya kukata tamaa ambayo tayari inawakabili maelfu ya raia wa Syria. Amesikitishwa na mashambulio mabaya yanayoshuhudiwa Ghouta Mashariki ambapo pia amesema Ujerumani inayalaani mashambulio hayo yanayofanywa na utawala wa Assad dhidi ya shule huku pia akiikosoa Urusi ambayo inayaangalia maovu hayo.
Katika siasa na matukio ya ndani ya Ujerumani kubwa linalozidi kuzungumziwa ambalo kansela hakuwa na budi ila kuweka sawa msimamo wake kama kiongozi wa nchi ni suala la ikiwa Uislamu ni sehemu au sio sehemu ya jamii ya Ujerumani. Merkel amesema hana shaka yoyote kwamba Uislamu ni sehemu ya jamii ya Ujerumani kama ambavyo pia Ukristo na uyahudi ni sehemu ya jamii za nchi hii. Ametaja kwamba Uislamu una haki kama dini nyingine nchini Ujerumani na ni sehemu ya nchi hii kwa kuzingatia ukweli kwamba kuwa waislamu milioni 4.5 wanaoishi Ujerumani.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Josephat Charo