1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel achaguliwa tena kuiongoza Ujerumani

Admin.WagnerD17 Desemba 2013

Bunge la Ujerumani limemuidhinisha tena Kansela Angela Merkel kuongoza serikali ya nchi hiyo kwa mara ya tatu, kufuatia makubaliano ya muungano na mahasimu wake wa kisiasa, chama cha kisoshalisti SPD.

https://p.dw.com/p/1AatQ
Kansela Angela MerkelPicha: Reuters

Siku 86 baada ya Merkel kupata ushindi katika uchaguzi, lakini akashindwa kupata wingi wa kujitosheleza bungeni,bunge la Ujerumani Bundestag limepiga kura kumpa muhula mwingine wa miaka minne. Tangu kumalizika kwa uchaguzi huo wa Septemba 22, Merkel mwenye umri wa miaka 59, amekuwa akifanya kazi kufikia makubaliano kati ya chama chake cha siasa za wastani za mrengo wa kulia CDU, ndugu zao kutoka jimbo la Bavaria CSU, na chama cha siasa za wastani za mrengo wa shoto SPD.

Waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer akimpongeza Merkel baada ya kuidhinishwa.
Waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer akimpongeza Merkel baada ya kuidhinishwa.Picha: Reuters

Wakiwa na jumla ya viti vya ubunge 504 kati ya 631, wahafidhina wa Merkel na washirika wao wapya wa SPD, wana wingi wa kutosha chini ya makubaliano yao ya muungano mkuu. Baada ya bunge ya kumuidhinisha, Merkel atakabidhiwa hati ya uthibitisho na rais wa shirikisho Joachim Gauck katika kasri la rais la Bellevue, kabla ya kurejea tena bungeni kuapishwa kama kansela wa tatu kushinda muhula wa tatu nchini Ujerumani tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia.

Kuanzia saa saba na nusu saa za hapa Ujerumani na kuendelea, wajumbe wa baraza jipya la mawaziri la Kansela Merkel watakabidhiwa vyeti vyao vya uteuzi, na vile vile kula viapo katika Bunge la Ujerumani.

Steinmeier amrithi Guido Westerwelle
Mawaziri hao wapya wanajumuisha waziri wa kazi Ursula von der Leyen kutoka chama cha CDU, ambaye atachukuwa usukani katika wizara ya ulinzi kutoka kwa Thomas de Maiziere, Wolfgang Schäuble, ambaye anaendelea na wadhifa wake wa waziri wa fedha, na waziri wa zamani wa mambo ya kigeni Frank-Walter Steinmeier - ambaye anarudi katika wadhifa huo alioushikilia kati ya mwaka 2005 hadi 2009.

Waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer akimpongeza Merkel baada ya kuidhinishwa.
Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel akimpongeza Merkel.Picha: Reuters

Baada ya kuapishwa kwa baraza jipya, mawaziri watafanya kikao chao cha kwanza rasmi, ambacho kimepangwa kufanyika saa 11 katika ofisi ya kansela. Merkel atalihutubia bunge kesho Jumatano, na kisha kusafiri kuelekea mjini Paris kwa ajili ya mazungumzo na rais Francois Hollande siku hiyo,kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mwishoni mwa wiki hii.

Merkel ametetea muda uliyotumika katika majadiliano ya kuunda muungano, hususan juu ya sera na nafasi za wizara kati yake na chama cha SPD, akisema siku ya Jumatatu baada ya kusainiwa kwa mkataba wa muungano kwamba walisikilizana. Hata hivyo, baadhi ya waangalizi wana wasiwasi kwamba kazi iliyoko mbele ya serikali mpya itakuwa ngumu.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae, afpe
Mhariri: Saum Yusuf