Juhudi tete za kuunda Serikali mpya ya Muungano
25 Septemba 2017Viongozi wa chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union (CDU) cha Kansela Merkel wamekutana leo asubuhi kutathimini matokeo ya uchaguzi mkuu ambapo chama chao kimejikingia asilimia 33 tu ya kura, kiwango cha chini kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1949; kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa leo asubuhi.
Ushindi huu wa nne mfululizo wa kansela Merkel aliyeko madarakani tangu mwaka 2005, ni mchungu kwake. Na dalili za mwanzo za malalamiko zimechomoza upande wa washirika wao wa kihafidhina wa Bavaria, Christian Social Union (CSU) wanaomhimiza Kansela Merkel aelemee zaidi mrengo wa kulia.
AFD washaanza kugombana
Kwa sababu sehemu ya wapigakura wa kihafidhina wamewapigia kura chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, Chaguo Mbadala kwa Ujerumani (AfD), kinachopinga wageni na waislam. "Baada ya miaka 12 madarakani, si rahisi kuibuka kuwa chama chenge nguvu zaidi. Lakini sasa changa moto kubwa iko mbele yetu. AfD wanawakilishwa bungeni. Tunataka kuwatanabahisha na kurejesha imani ya wale waliowapigia kura kwa kuzingatia kwa makini zaidi madai yao na kwa kuiendesha nchi vyema zaidi."
AfD wamejikingia asilimia 12.6 ya kura kwa kufanya kampeni wakimuigiza rais wa Marekani Donald Trump na kushadidia msimamo wa Uingereza wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya.
Ufa umejitokeza miongoni mwa viongozi wa AfD kuhusu msimamo unaobidi kufuatwa na chama hicho. Mwenyekiti mweza wa chama hicho, Frauke Petry, amesema leo hatoketi na wafuasi wengine wa chama hicho bungeni akilalamika dhidi ya msimamo mkali wa mrengo wa kulia unaofuatwa na wenzake.
CSU kinazingatia uwezekano wa kuunda kundi lake bungeni
Mbali na juhudi za kurejesha imani ya wapiga kura waliokipa kisogo chama cha CDU, kansela Merkel anakabiliwa na kishindo chengine pia, mwenyekiti wa chama ndugu cha kusini mwa Ujerumani, CSU, Horst Seehofer, anazungumzia uwezekano wa kutowakilishwa na kundi moja katika bunge la shirikisho, Bundsetag.
Baada ya SPD kuamua kukalia viti vya upinzani bungeni, Kansela Merkel amebakiwa na njia moja tu; kuunda serikali ya muungano ambayo haijawahi kushuhudiwa humu nchini, kati ya vyama vya kihafidhina vya CDU/CSU, waliberali wa FDP na Walinzi wa Mazingira (die Grüne).
Mazungumzo ya kuunda serikali yanaweza kudumu miezi kadhaa na pindi yakishindwa kuleta tija, uchaguzi mpya utaitishwa.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/dpa/afp/AP
Mhariri: Yusuf Saumu