1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MELILLA : Wahamiaji wa Kiafrika kwa mara nyengine wakimbilia katika eneo la Uhispania lilioko ndani ya Morroco

3 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CEVM

Wahamiaji wa Kiafrika kwa mara nyengine tena wamevuka mpaka wa Morroco na kukimbilia kwenye eneo la Uhispania liliomo ndani ya ardhi ya Morroco la Melilla kabla ya alfajiri leo hii licha ya kuongezeka kwa hatua za usalama kufuatia wimbi la wahamiaji waliojaribu kuingia humo wiki iliopita.

Ingawa wizara ya mambo ya ndani haikutowa idadi ya wahamiaji hao lakini repoti za vyombo vya habari zinasema mamia ya wahamiaji walijaribu kuvuka na wengi walifanikiwa.Televisheni ya taifa ya Uhispania imesema wale waliofanikiwa kukimbia wanafikia 300.

Leo asubuhi kituo cha polisi huko Melilla kilionekana kujaa Waafrika ambao walifika hapo kujisalimisha baada ya kuvuka uzio mbili za sen’gen’ge zinazotenganisha eneo hilo la Melilla na Morroco.

Maafisa wa chama cha Msalaba Mwekundu wamesema watu wanaofikia 200 waliweza kuvuka mpaka huo ambao uliimarishwa kwa vikosi vya wanajeshi baada ya watu wanaokadiriwa kufikia 1,000 kutumia ngazi kujaribu kuruka sen’gen’ge hizo hapo Jumanne iliopita na 300 kati yao kufaulu.