1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meli ya Costa Allegra yavutwa katika eneo salama

MjahidA28 Februari 2012

Meli ya kifahari ya Italia ilio na zaidi ya abiria 1000 inavutwa katika eneo salama na mashua ya kifaransa, baada ya moto kuzuka katika chumba cha nyaya katika meli hiyo na kuteketeza mitambo yake ya kuzalisha umeme.

https://p.dw.com/p/14B9z
Meli ya kifahari ya Costa Allegra
Meli ya kifahari ya Costa AllegraPicha: dapd

Meli hiyo Costa Allegra inavutwa kuelekea kisiwa cha Desroches, kilomita 240 Kusini Magharibi mwa Ushelisheli katika kisiwa cha Mahe. Maafisa wa usalama wanasema moto uliozuka katika meli hiyo ya Costa Allegra ulifanikiwa kuzimwa na hakuna mtu yoyote aliyejerihiwa katika mkasa huo. Hata hivyo mashua mbili za uvuvi kutoka kisiwa cha Ushelisheli zinaelekea katika meli hiyo na zinatarajiwa kufika hii leo mchana. Meli ya Costa Allegra, ina abiria 636 na wafanyikazi 413. Kati ya abiria hao wanne ni watoto wadogo chini ya miaka minne.

Mashua moja ya uvuvi kutoka Ufaransa tayari imefikia Meli ya Costa Allegra. Serikali ya Ushelisheli imesema inafanya mipango ya kuwahamisha abiria kutoka katika meli hiyo hadi katika kisiwa cha Mahe. Mashua hiyo imebeba genereta, chakula, na simu za mawasiliano za redio.

Aidha wahandisi 15 wanaelekea katika kisiwa cha mahe ili kuitengeneza meli hiyo.

Moto uliozuka jana katika Coata Allegra ulizua wasi wasi mkubwa hasaa ikizingatiwa kwamba, ni wiki sita tu baada ya meli kama hiyo Costa Concordia kupinduka katika bahari ya Italia na kusababisha vifo vya watu takriban 25 huku wengine 7 wakiwa hawajulikani waliko. Meli zote mbili Costa Allegra na Coasta Concordia zinamilikiwa na kampuni moja.

Maharamia wa kisomali
Maharamia wa kisomaliPicha: picture alliance / dpa

Costa Allegra ilioondoka kutokea kaskazini mwa Madagascar ilikuwa inaelekea katika bandari ya Victoria mji mkuu wa Ushelisheli.

Hata hivyo mkurugenzi wa kampuni ya meli hiyo Giorgio Moretti amesema uchunguzi wa kubaini chanzo cha moto huo unaendelea. Kwa sasa battery za umeume za dharura ndio zinazoendesha meli hiyo, na kuwezesha mawasiliano ya radio ndani ya Costa Allegra. Abiria wote katika meli hiyo wamewekwa katika chumba kimoja kikubwa.

Eneo ambapo meli hiyo imekwama katika bahari hindi ni ngome maarufu ya maharamia wa kisomali na imeshuhudia mashambulizi tofauti za maharamia hao. Mwaka wa 2009 meli moja ya Italia iliokuwa na abiria 1,500 ilishambuliwa na maharamia katika pwani ya Somalia. lakini taarifa zinasema kwamba hadi sasa hakuna dalili zozote za maharamia walioonekana karibu na meli hiyo.

Mwandishi Amina Abubakar /AP/dpa

Mhariri Sekione Kitojo