Meles Zenawi afariki dunia
21 Agosti 2012Legesse Zenawi alizaliwa tarehe 8 mwezi Mei mwaka 1955. Baba yake alikuwa mkulima mdogo aliyeishi huko Adua, kaskazini mwa Ethiopia. Baadaye alipewa jina la "Meles", jina hilo likimuenzi mpigania uhuru mmoja. Alihitimu kutoka shule ya watu wenye vipaji maalumu na kupata shahada mbili za uzamili, akisoma kwa njia ya posta. Elimu aliyoipata, ilimpa nafasi ya kutoa hotuba za kitaaluma mbele ya wageni wa serikali ya nchi yake.
Alipokuwa akisomea udaktari, Meles (anayeitwa kwa jina lake la kwanza kama ilivyo ada nchini Ethiopia), alianza kujihusisha na mausala ya kisiasa. Alijiunga na makundi yanayofuata mafundisho ya mwanafalsafa Karl Marx. Aliungana pia na vuguvugu lililosababisha kung'olewa madarakani kwa mfalme Haile Selassie mwaka 1974.
Muasi awa Waziri Mkuu
Baada ya Mengistu Haile Mariam kuingia madarakani, Meles alikatisha masomo yake na badala yake kuingia katika vita vya chini kwa chini dhidi ya Mengistu. Kwa zaidi ya miaka 10, kundi lake la waasi liitwalo Tigray's People Liberation Front (TPLF), lilifanya mashambulizi katika milima ya Tigray. Mwezi Mei 1991, waasi wa kundi la TPLF, wakisaidiwa na Marekani, walifanikiwa kuuteka mji mkuu Addis Ababa. Meles, aliyekuwa rais wa kipindi cha mpito, alipoulizwa na gazeti la hapa Ujerumani la Frankfurter Rundschau kama nchi yake iko tayari kwa demokrasia alijibu: "Hivi mnafahamu kwamba nchi yetu ilikuwa na utamaduni ulioendelea kabisa wakati ninyi mlikuwa bado wawindaji na watu wakukusanya matunda na mboga msituni?"
Meles alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia. Muungano wa vyama uliokuwa madarakani tangu mwaka 1991, Ethiopian Peoples' Revolutionary Democratic Front (EPRDF), ulianza kuwasaka washirika wa Mengistu. Tangu kuingia madarakani kwa Meles, mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakilaani sera zake, hasa juu ya namna alivyoiendesha nchi yake katika miaka ya 1990 lilipotokea janga la njaa.
Mfano bora wa mwanzo mpya barani Afrika?
Matukio mawili makuu yalimaliza kabisa dhana kwamba Meles ndiye tumaini la mwanzo mpya Afrika: Tukio la kwanza ni vita kati ya Ethiopia na nchi jirani ya Eritrea, vilivyotokea kati ya mwaka 1998 na 2000. Tukio la pili ni wizi wa kura katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2005. Watu wapatao 200 waliuwawa kwenye maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo. Wakati Meles alipokuwa akijisifu kwa kuwapataia raia wake haki ya kufanya uchaguzi aliouita wa haki, maafisa wake wa usalama waliwashambulia kwa risasi wanafunzi waliokuwa wakiandamana na kuwaua.
Baada ya uchaguzi wa mwaka 2005, mashirika ya kutetea haki za binadamu yaliripoti juu ya rushwa na matumizi ya nguvu dhidi ya wapinzani. Tarehe 12 Juni mwaka 2012, waandishi wa habari, wapinzani na wanaharakati 24 walihukumiwa chini ya sheria mpya ya kupambana na ugaidi. Mwandishi mmoja wa blogu alihukumiwa kifungo cha miaka 18. Utawala wa Meles unashutumiwa pia kwa kutumia fedha za misaada kwa ajili ya kampeni ya uchaguzi.
Kiongozi mwenye sura mbili
Meles, ambaye alikuwa anapendelea kusoma, kuogelea au kucheza tenisi katika muda wake wa mapumziko, alikuwa na kipaji cha kuzungumza mbele za watu. Kipaji hicho kinaonyesha pande mbili za kiongozi huyu. Nchini mwake alikuwa kingozi asiyesita kuzima upinzani wowote dhidi yake, ikibidi hata kwa kutumia nguvu. Lakini katika majukwaa ya kimataifa alijionyesha kuwa msemaji wa bara la Afrika, akizungumzia masuala kama vile mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kwa bara la Afrika.
Hata hivyo yapo mambo ya maendeleo aliyowaletea wananchi wake, maendeleo katika sekta ya elimu na sekta ya afya yakiwa miongoni mwa hayo. Kiujumla, Ethiopia ilijipatia maendeleo mengi chini ya utawala wake, licha ya kwamba maendeleo mengi yalikwamishwa na ongezeko la kasi la idadi ya watu nchini humo. Hata uchumi wa Ethiopia unakua kwa haraka, lakini wanaofaidika zaidi ni viongozi wa kisiasa.
Afya ya Meles
Kwa muda mwingi kumekuwepo na tetesi juu ya kuugua kwa Meles. Mara kwa mara kiongozi huyo alilazimika kwenda nje ya nchi kwa matibabu. Aliposhindwa kuhudhuria mkutano mkuu wa Umoja wa Afrika uliofanyika Julai 2012 mjini Addis Ababa, ulizuka uvumi juu ya kifo chake. Hata hivyo, msemaji wake alikanusha taarifa hizo.
Meles Zenawi alifariki dunia Jumanne, 21.08.2012. Amemwacha mke wake Azeb Mesfin na watoto watatu.
Mwandishi: Ludger Schadomsky
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Josephat Charo