Mechi ya Denmark na Finland EURO 2020 yaanza tena
12 Juni 2021Awali mechi hiyo ilisitishwa kwa muda baada ya mchezaji wa timu ya Denmark Christian Eriksen kuanguka na kupoteza fahamu uwanjani wakati wa mechi yao ya kundi B na Finland kwenye michuano ya kombe la EURO 2020.
Tukio hilo lilitokea kuelekea mwisho wa kipindi cha kwanza dakika ya 42 wakati mchezaji huyo wa umri wa miaka 29 alipodondoka chini.
Madaktari wa timu ya Denmark walikimbia haraka uwanjani kwenda kumtibu Eriksen, ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya Inter Milan katika ligi ya Serie A nchini Italia. Wachezaji wenzake walimzunguka wakati madaktari walipojaribu kumsaidia azinduke kutumia utaalamu wa CPR kwa kiungo huyo wa zamani wa Tottenham wakati alipokuwa amelala chini.
Matibabu yaliendelea uwanjani kwa zaidi ya dakika 15 kabla Eriksen kubebwa kwenye machela na kuondolewa uwanjani. Mpigapicha wa shirika la habari la Reuters amesema amemuona Eriksen akiinua mkono wake alipokuwa kwenye machela akiondolewa uwanjani.
Timu zote mbili baadaye ziliondoka uwanjani kuelekea vyumba vya kubadilishia nguo, huku maafisa wakiinua nguo juu kuzuia Eriksen asionekane.
Kiungo huyo mchezeshaji ndiye mfungaji bora wa magoli wa Denmark katika mechi za kufuzu kwa mashindano ya EURO 2020, akifunga mabao 5.
Reuters, AP