MECCA.Viongozi wa Hamas na Fatah waendelea na mazungumzo mjini Makka
7 Februari 2007Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas na viongozi wa Hamas wanaendelea na mazungumzo ya kumaliza mgogoro baina ya vyama vyao katika mji mtakatifu wa Mecca nchini Saudi Arabia.
Abbas anaekiongoza chama cha Fatah na waziri mkuu wa Paletina Ismail Haniya akiwa pamoja na kiongozi wa kundi la Hamas mwenye makao yake nchini Syria Khaled Meshaal wanazungumzia juu ya uwezekano wa kuundwa kwa serikali ya umoja ya Palestina.
Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia aliyeandaa mkutano huo amezihimiza pande hizo mbili kufikia maelewano ili kuepuka vita.
Kabla ya mkutano huo kuanza waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert alitangaza kuwa atakutana na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice baadae mwezi huu katika mji wa Jerusalem nchini Israel.