Mdudu anayepaa Kilomita 6,000
20 Mei 2016Sijui kama umeshapata kusikia mdudu anayeitwa kurumbiza au kereng'ende? Huyu ni aina ya mdudu ambaye ni maarufu sana aakiwa na uwezo wa kuruka au kupaa kilomita nyingi. Inatajwa kwamba kurumbiza katika kipindi cha uhai wao wanaweza kupaa kwa takriban kilomita 6,000 kwenda na kurudi.
Utafiti uliofanywa na kituo kinachohusika na kufuatilia wadudu wanaohama sehemu moja kwenda nyingine kilichoko Marekani baada ya kuwachunguza wadudu hao kutoka nchi sita za mabara tafauti, umegundua kwamba vinasaba vya wadudu hawa licha ya kutokea umbali mkubwa havitofautiani kwa kiasi kikubwa. Na kwa maana hii wadudu hawa kutokana na uwezo wao wa kuzunguka masafa marefu sana duniani wanakuwa na umoja na ukaribu sana kama familia, linasema shirika la Plos One katika utafiti huo. Inasemekana kurumbiza hutoka India kila mwaka na kufanya ziara hadi Afrika na katika safari hiyo hawatumii njia ya ardhi bali wanavuka Bahari ya Maldives na Bahari ya Hindi.
Mwandishi: Saumu Mwasimba