1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mdahalo kati ya dini wafunguliwa Madrid Uhispania

Nijimbere, Gregoire17 Julai 2008

Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia, ameufungua mdahalo kati ya dini akitoa mwito wa kupambana na hitikadi kali zinazochafua dini. Safari hii mdahalo huo unaelekezwa kwa maridhiano badala ya tofauti kati ya dini.

https://p.dw.com/p/Ee6N
Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia akipokewa na Baba Mtakatifu Benedicto wa XVI huko Vatican Italy mwaka jana.Picha: AP

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa mdahalo huo, Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia, amesema ´´Sisi sote tunamuabudu Mungu moja na tumekutana kusema ya kwamba dini zinatakiwa kuwa na maridhiano badala ya kuwa na tofauti´´, amesisitiza Mfalme Abdullah, kiongozi wa nchi ambako viongozi wa madhehebu ya Wahhabi wana ushawishi mkubwa kwa familia ya kifalme na pia nchi iliochafuliwa na mashambulizi ya Setemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani ambapo watu 15 miongoni mwa wale 19 walioshiriki kuziteka nyara ndege za Marekani ni kutoka Saudi Arabia. Mfalme Abdullah amesema analeta ujumbe wa waislamu kwa jumla.

Hii ni mara ya kwanza Saudi Arabia kuandaa mkutano kama huo, nchi ambako waumini wa dini nyingine mbali na Islamu hawana haki ya kudhihirisha dini lao hadharani, sababu ambayo wadadisi wa mambo ya kidini wamesema, imepelekea mkutano huo kutoandaliwa nchini Saudi Arabia kuepusha kile wamekitaja ´´mjadala mkubwa`´. Wajumbe kiasi ya 200 wa dini za kiislamu, kikristu na kiyahudi kutoka pembe nne za dunia wanashiriki. Wanashiriki pia wawakilishi wa dini nyingine kama Budha, Hindu na Sikh. Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair na Kasisi Jesse Jeckson kutoka Marekani ni miongoni wa waalikwa.

Mfalme wa Uhispania Juan Carlos, ametoa muelekeo wa mdahalo huo yaani kuleta maridhiano: ´´Mdahalo unabidi kuelekezwa katika kuheshimu kila upande na imani zetu lazima zielekezwe katika juhudi za kujuana vizuri zaidi. Pia tunapenda kusisitiza juu ya kuwepo maadili ya kushirikiana na kuelewana´´.

Na ili kuzidi kuelewana, inabidi wabadili pia maada katika mdahalo. Kwani ameelezea Mfalme Abdullah, midahalo kati ya dini iliotangulia ilishindwa kufikia ufanisi kutokana na kwamba walioshiriki walitilia mbele tofauti zao na kuendeleza mtafaruku kati yao.

Katibu mkuu wa Baraza la kiyahudi duniani Michael Schneider amekaribisha kongamano hilo ambalo limeandaliwa baada ya Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia kukutana kwa mazungumzo na kiongozi wa kanisa la kikatoliki duniani Baba Mtakatifu Benedicto wa XVI huko Vatican mjini Roma Italy mwezi Novemba mwaka jana. Wawakilishi wa kiyahudi na kikristu katika mkutano huo, wamesema Mfalme Abdullah ameonyesha nia njema ya kupambana na imani kali za kidini ambazo zimeshasababisha majanga kadhaa duniani.