1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchuano wa watani wa Madrid mjini Lisbon

23 Mei 2014

Hakutakuwa na mapenzi yoyote kati ya majirani wawili wakati wachezaji wa Real Madrid na Atletico Madrid watakaposhuka dimbani katika fainali ya Champions League mjini Lisbon, Ureno.

https://p.dw.com/p/1C5L0
Real Madrid vs. Atletico Madrid Spanien Liga Primera Division
Picha: picture-alliance/dpa

Timu hizo za Uhispania zinakutana katika fainali ya kwanza katika historia ya Champions League baina ya mahasimu wawili wa mji mmoja. Real Madrid ndiyo timu iliyopata mafanikio mengi katika kinyang'anyiro hicho na inalenga kumaliza subira ya miaka 12 ya kunyakua taji la kumi la Ulaya maarufu kama “La Decima”. Lakini Atletico ambao wamedhihirisha kuwa wachafuaji wakubwa msimu huu, baada ya kuwapiku Barcelona katika taji la La liga wikendi iliyopita na sasa wanasalia na mchuano mmoja pekee ili kuukamilisha msimu wenye mafanikio makubwa kabisa katika historia ya miaka 111 ya klabu hiyo.

Cristiano Ronaldo anatarajiwa kurejea katika kikosi cha Real kutoka mkekani, lakini bado tunasubiri kuona kama kocha wa Atletico Diego Simeone atampa fursa mshambuliaji Diego Costa ambaye amefanya mazoezi jana. Kurejea kwa Ronaldo kutaimarisha hata zaidi safu ya mashambulizi makali ya Madrid huku Gareth Bale akitarajiwa kuanza. Lakini mshambuliaji Karim Benzema anatiliwa shaka kwa sababu ya jeraha. Pia beki Pepe huenda akakosa kuanza.

Cristiano Ronaldo ataongoza mashambulizi ya Real Madrid
CR7 ataongoza safu ya mashambulizi ya Real MadridPicha: Getty Images

Kukosekana kwa Xabi Alonso ni pigo kubwa kwa safu ya kiungo ya Madrid. Mhispania huyo amekuwa mojawapo ya wachezaji ambao ni nguzo muhimu katika timu ya Carlo Ancelotti msimu huu, lakini kadi ya njano katika nusu fainali dhidi ya Bayern Munich imemweka nje ya fainali. Mmoja kati ya Sami Khedira, Asier Illaramendi au Casamiro anatarajiwa kupewa kibali cha kujaza pengo hilo na kuchukua mzigo wa kuyafungua mashambulizi ya Madrid na kuvunja mchezo wa Atletico.

Uwezo wa kufunga magoli wa David Villa unaweza kuziba pengo la Diego Costa kama hatokuwepo lakini uzoefu wa mchezaji huo wa Uhispania hautatosha kuisaidia Atletico ambayo inakosa uzoefu katika Champions League.

FC Barcelona gegen Atletico Madrid
Diego Simeone amewashangaza wengi kutokana na mafanikio ya Atletico Madrid msimu huuPicha: picture-alliance/dpa

Madrid wanaweza kutegemea uzoefu wa CR 7 na Iker Casillas katika Champions League. Kocha Carlo Ancelotti ameweza kuifikisha Madrid mahali ambako Jose Mourinho hangeweza, na sasa Muitaliano hup anasalia na ushindi mmoja pekee akiifikia rekodi ya Bob Paisley kwa kunyakua kombe lake la tatu la Ulaya.

Mwenzake Diego Simeone huenda akawa kocha wa tatu asiye raia wa Ulaya kushinda kombe hilo. Wengine wawili waliowahi kunyakua taji hilo ni Luis Carniglia wa Real mwaka wa 1958 na 59, na Helenio Herrera wa Inter Milan mwaka wa 1994 na 65.

Mchuano huo ndio derby muhimu kabisa ya Madrid baada ya michezo 194 ya ligi na Kombe la Shirikisho la Soka Uhispania. Madrid ina faida ya ushindi 102 dhidi ya 46 wake Atletico. Msimu uliopita Atletico waliwapiku Real katika fainali ya Kombe la Mfalme katika uwanja wa Santiago Bernabeu.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Mohammed Khelef