Mchezaji wa kutoka China awa shujaa katika Derby Catalonia
6 Januari 2020Bao la dakika za mwisho la kusawazisha kwa Espanyol dhidi ya Barcelona liliashiria ukurasa mpya katika kandanda la Uchina, vyombo vya habari vya nchi hiyo vilisema jana, baada ya tukio hilo la kishujaa kusambaa mitandaoni nchini humo.
Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya China Wu Lei aliingia dimbani akitokea benchi na kupachika bao katika dakika ya 88 ambalo lilileta sare ya mabao 2-2 kwa timu hiyo iliyochini ya msimamo wa ligi ya La Liga katika pambano la watani wa jadi, derby, siku ya Jumamosi.
Ushindi mfululizo wa michezo mitano wa Real Sociedad ulifikia mwisho jana katika ligi ya Uhispania baada ya kupata kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Villarreal na kupoteza mwelekeo katika mbio za kupata nafasi katika champions League.
Barcelona na Real Madrid zinafungana juu ya msimamo wa ligi zikiwa na pointi 40 kila moja, ambapo klabu hiyo kutoka jimbo la Catalonia iko mbele kwa tofauti ya magoli.
Wakati huo huo mashindano ya Super Cup nchini Uhispania yaliyopewa msukumo mpya yanaaza siku ya Jumatano nchini Saudi Arabia, hatua ambayo itaongeza kipato kwa shirikisho la kandanda nchini humo lakini imeyakasirisha makundi ya haki za binadamu na mashabiki nchini humo. Real madrid na Valencia zinakutana katika nusu fainali ya kwanza mjini Jeddah siku ya Jumatano kabla ya barcelona kupambana na Atletico Madrid masaa 24 baadaye siku ya Alhamis, fainali itafanyika siku ya Jumapili.
Super Cup ilikuwa ni mchezo wenye mikondo miwili kati ya mabingwa wa ligi na kombe la taifa Copa del Rey lakini mkuu wa shirikisho la kandanda Luis Rubiales aliendesha mabadiliko makubwa Novemba mwaka jana , akipata makubaliano ya miaka miwili kuchezesha mashindano hayo nchini saudi Arabia.