Mchakato waanza kumpata waziri mkuu Japan
8 Septemba 2020Suga katibu mkuu wa baraza la mawaziri, mwenye umri wa miaka 71 mtoto wa mkulima, tayari amepata uungwaji mkono wa makundi muhimu katika chama cha Liberal Democratic kabla ya uchaguzi wa kiongozi wa chama hapo Septemba 14.
Lakini Suga hagombei bila kupingwa, ambapo waziri maarufu wa zamani wa ulinzi na mkuu wa sera za chama anagombea dhidi yake.
Wakati chama cha LDP kina wingi wa kutosha bungeni, mshindi wa mbio hizo ana hakika ya kushinda kura bungeni hapo Septemba 16 na kuteuliwa kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo.
Mbio za kumpata waziri mkuu mpya kutoka chama cha LDP zilianza, baada ya waziri mkuu aliyehudumu kwa kipindi kirefu nchini Japan Shinzo Abe, ghafla alitangaza mwishoni mwa mwezi Agosti kuwa atajiuzulu kutokana na sababu za kiafya.
Kuna uvumi kwamba kiongozi mpya pia anaweza kuitisha uchaguzi wa mapema kuvutia uungwaji mkono wa umma.
Leo asubuhi , wawakilishi wa Suga na mahasimu wake, waziri wa zamani wa ulinzi Shigeru Ishiba na mkuu wa sera za chama Fumio kishida, rasmi wamejiandikisha kuwa wagombea.
Uchaguzi na mapema
Wagombea wanatarajiwa kutoa hotuba na kuwa na mkutano wa pamoja na waandishi habari baadaye leo.
Pia kutakuwa na midahalo miwili , licha ya kwamba upigaji kura utakuwa wa wabunge wa chama cha LDP pekee na wawakilishi watatu wa chama kutoka kila jimbo la Japan katika majimbo 47. Kura pana zaidi itakayojumuisha wanachama wote haitafanyika, ambapo maafisa wanasema itachukua muda mrefu zaidi kutayarisha.
Yeyote atakayechukua uongozi wa ofisi hiyo ya juu kabisa katika uongozi nchini Japan atakabiliwa na changamoto kadhaa, kuanzia janga la virusi vya corona pamoja na kuuweka vizuri uchumi wa nchi hiyo na kuhakikisha michezo ya Olimpiki ya Tokyo iliyoahirishwa inafanyika.
hakuna miongoni mwa wagombea hao watatu anayeonekana kutoa uwanja wa sera ambao utatofautiana kwa kiasi kikubwa kutoka zile za Abe, ambapo Yoshihide Suga amesema wazi kwamba anapanga kuendeleza mipango ya waziri mkuu anayeondoka madarakani.
"Nimeamua kugombea katika uchaguzi wa chama cha Liberal democratic LDP. Naahidi kufuata sera ambazo waziri mkuu Abe amejitolea mwili na moyo wake kuzisukuma mbele. Na ili kuzisogeza mbele zaidi, nina nia ya kujitoa kuzitekeleza."
Ishiba na Kishida wote wamezungumzia haja ya kuhakikisha kuwa kichocheo uchumi kilichotolewa baada ya mzozo wa virusi vya corona vinalenga wale wenye uhitaji. Ishiba ambaye ni mfanyakazi wa zamani wa benki , mwenye umri wa miaka 63 ni maarufu kwa wapiga kura na mara kadhaa amekuwa akionekana kuwa chaguo la wapiga kura kabla ya kujiuzulu kwa Abe.