Mchakato wa Wilders kutafuta washirika Uholanzi wavurugika
27 Novemba 2023Kuondoka kwa Gom van Strien, seneta kutoka chama cha Wilders cha Freedom Party kuhusiana na madai ya udanganyifu kumeuparaganyisha mchakato wa kuunda serikali mpya kabla hata haujaanza. Van Strien aliteuliwa wiki iliyopita kama "skauti" kujadili uwezekano wa kuunda muungano.
Alipangiwa kukutana na Wilders na viongozi wengine wa chama siku ya Jumatatu, lakini mikutano hiyo yote imefutwa. "Inakasirisha kuanza awamu ya mazungumzo ya mwanzo kwa namna hii," Vera Bergkamp, rais wa baraza la chini la bunge la Uholanzi, alisema katika taarifa.
Aliongeza kuwa "hivi sasa ni muhimu kwamba skauti mpya anateuliwa haraka ambaye anaweza kuanza kazi mara moja.
Soma pia:Wilders ashinda uchaguzi kwa kishindo Uholanzi
Van Strien amekana kufanya makosa yoyote baada ya vyombo vya habari vya Uholanzi kuripoti kwamba alikuwa anakabiliwa na kesi ya udanganyifu. Lakini siku ya Jumatatu asubuhi, alitoa taarifa akisema kwamba "msukosukom ulioibuka kuhusu hili na maandalizi ya majibu juu yake" vimekwamisha kazi yake ya kutafuta washirika wa muungano.
Van Strien ni seneta mwenye uzoefu mkubwa lakini asiefahamika sana kutoka chama cha Wilders, kinachofahamika kwa kifupi chake cha Kidachi PVV.
Alikuwa ametwikwa jukumu la kuandaa orodha ya vyama vinavyoweza kuwa washirika wa muungano na kuripoti katika baraza la chini la bunge la Uholanzi ifikapo mapema Desemba, ili wabunge waweze kujadili suala hilo mnamo Desemba 6 kabla ya kumteua afisa mwingine kuanza mazungumzo thabiti zaidi ya kuunda muungano.
Changamoto zinazomkabili Wilders za PVV
Chama cha Wilders cha PVV ndiyo mshindi wa kushtukiza wa uchaguzi wa wiki iliyopita, katika mabadiliko ya kustajabisha kuelekea mrengo mkali wa kulia katika siasa za Uholanzi ambao umesababisha mtikisiko kote barani Ulaya. Wilders ambaye kwa muda mrefu amekuwa mtu wa nje na akitengwa na vyama vikubwa, hivi sasa yuko katika msitari wa mbele kuunda muungano tawala.
Hata hivyo, matumaini yake ya kuunda haraka muungano wa mrengo wa kulia yalipata pigo wiki iliyopita baada ya Dilan Yesilgöz-Zegerius, kiongozi mpya wa chama kikuu cha mrengo wa kulia cha VVDcha Waziri Mkuu anayeondoka Mark Rutte, kusema chama chake hakitajiunga na muungano unaoongozwa na PVV.
Licha ya kumkatalia, Wilders amemhimiza Yesilgöz-Zegerius kuungana naye katika mazungumzo ya muungano na kiongozi wa vyama viwili vipya vilivyopata mafanikio makubwa katika uchaguzi huo, chama cha msimamo wa kati cha New Social Contract na chama cha Vuguvugu la Wakulima.
Soma pia:Chama cha siasa kali Uholanzi chajipanga kuunda serikali
Kujiuzulu kwa Van Strien kunaangazia moja ya masuala muhimu ambayo Wilders huenda akakabiliana nayo wiki zijazo wakati kundi lake la wabunge wapya wakichukua viti vyao bungeni - ukosefu wa uzoefu wa kisiasa katika chama chake.
Chama cha PVV wakati wote kimekuwa kikitegemea umaarufu wa Wilders, ambaye hupanga sera na ni mojawapo ya sura chache zinazotambulika hadharani za chama.