1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato wa rufaa ya kesi ya BBI waanza

29 Juni 2021

Mchakato wa kukata rufaa kesi ya BBI iliyotupwa nje na mahakama kuu na kusitisha shughuli ya kuandaa kura ya maoni umeanza Jumanne.

https://p.dw.com/p/3vlEh
Kenia Präsident Uhuru Kenyatta und Oppositionsführer Raila Odinga in Nairobi
Picha: Reuters/T. Mukoya

Kulingana na mahakama kuu mpango wa maridhiano wa BBI na kura ya maoni unakiuka katiba kwani haukuushirikisha umma kwa njia iliyo sawa. Majaji wa mahakama ya rufaa wana muda wa hadi siku ya Ijumaa kuisikiliza kesi hiyo na kisha kuandaa uamuzi wao.

Jopo la majaji saba linaloongozwa na rais wa mahakama ya rufaa Daniel Musinga lilianza asubuhi ya Jumanne kusikiliza kesi ya mchakato wa BBI unaoazimia kuipisha kura ya maoni na mageuzi ya katiba.

Majaji wanaosikiliza kesi

Jaji Musinga na wenzake Roselyne Nambuye, Hannah Okwengu, Patrick Kiage, Gatembu Kairu, Fatuma Sichale na Francis Tuyoitt ndio wanaosikiliza kesi hiyo.

Rufaa hii imewasilishwa na Rais Uhuru Kenyatta, Kiongozi wa ODM Raila Odinga na sekretarieti ya BBI, Mwanasheria Mkuu pamoja na Tume ya Uchaguzi na Mipaka IEBC.

James Orengo ambaye pia ni Seneta wa Siaya alimwakilisha Raila Odinga wa chama cha ODM. Kwa upande wake mwanasheria mkuu anawashirikisha wanasheria Paul Nyamodi na Kamau Karori pamoja na Wakili Mkuu wa serikali Kennedy Ogeto.

Kenia Präsident William Ruto
Makamu wa Rais wa Kenya, William RutoPicha: picture-alliance/Photoshot/P. Siwei

Mapema Jumanne Ogeto aliwasilisha hoja tisa ambazo watajikita hapo ili kuishawishi mahakama ya rufaa kuubatilisha uamuzi wa mahakama kuu ulioufutilia mbali mpango wa BBI na kura ya maoni.

Ogeto aliwakosoa majaji watano waliosikiliza kesi hiyo ya BBI kwa kutumia maelezo ya kamusi la mtandaoni la Wikipedia kwenye suala la kuushirikisha umma.

Wakili Kamau Karori wa upande wa mwanasheria mkuu alisisitiza kuwa mahakama kuu ilifanya kosa mintarafu suala la kukusanya saini kwani iliegemea zaidi mchakato badala ya matokeo.

Mchakato wa BBI ulikiuka katiba

Itakumbukwa kuwa Mei 17 jopo hilo la majaji watano liliamuru kuwa mchakato wa BBI ulikiuka katiba na kuibana tume ya IEBC kuandaa kura ya maoni kabla ya kuushirikisha umma kikamilifu.

Kwa mtazamo wa wataalam wa sheria, uamuzi wa jopo la majaji saba wa mahakama ya rufaa huenda ukaambulia kwenye mahakama ya juu zaidi.

Naibu wa Rais William Ruto na washirika wake wa karibu wanashikilia kuwa muda hauruhusu kufanya kura ya maoni kwani dhoruba za COVID-19 zimewavuruga wananchi.

Jopo la majaji saba wa mahakama ya rufaa lina muda hadi Ijumaa kusikiliza hoja za pande zote na baada ya hapo kuandaa uamuzi wao iwapo kauli ya mahakama kuu itabatilishwa au la.