Mchakato wa kumpata mgombea mwenza wa Raila
21 Aprili 2022Tume ya uchaguzi nchini humo, IEBC imewapa wagombea wa urais hadi Alhamisi ijayo kutangaza wagombea wenza wao. Kwenye kongamano la mapema hii leo, baraza kuu la muungano wa Azimio One Kenya lilizindua rasmi mchakato wa kumsaka mgombea mwenza wa Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 mwaka huu.Kwa mujibu wa katibu mkuu wa baraza hilo, Junet Mohammed, jopo maalum la ushauri linaundwa kuwateua watakaowawakilisha katika uchaguzi ujao.
Hata hivyo tarehe kamili ya tangazo hilo muhimu haijakuwa bayana.Kikao cha leo kilichoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta kwenye jumba la mikutano la KICC kimeridhia pia kuunda vyombo maalum vya uongozi wa muungano.Vyombo hivyo ni pamoja na bodi ya uchaguzi,bodi ya rufaa ya uchaguzi,kamati ya taifa ya nidhamu na jopo la kusuluhisha mizozo.
Majina yanayotajwa
Kamati kuu ya muungano ndiyo itakayokuwa na wajibu wa kuwasilisha majina ya watakaoongoza taasisi hizo.Mkutano wa leo uliwaleta pamoja pia kiongozi wa Wiper Democratic Kalonzo Musyoka,Mwenyekiti wa chama cha KANU Gideon Moi,kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, Charity Ngilu wa Narc aliyepia gavana wa Kitui na Wafula Wamunyinyi wa DAP-K. Mbunge wa Taveta, Naomi Shaban na mwakilishi wa wanawake wa kaunti ya Muranga Sabina Chege pia walihudhuria kikao hicho.
Soma pia→Wakenya kuhusu uamuzi wa mahakama kutupa nje mchakato wa BBI
Je, wanawake wananafasi hiyo ?
Ifahamike kuwa viongozi wanawake katika muungano wa Azimio One Kenya wamekuwa mstari wa mbele kusukuma hoja ya mwanamke kuteuliwa kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9. Rachel Shebesh ni katibu mwandamizi katika wizara ya Jinsia na mwakilishi wa kwanza wa wanawake katika kaunti ya nairobi.
Yote hayo yakiendelea, Chama cha UDA cha Naibu wa Rais William Ruto kinajiandaa kwa mkutano wa siku mbili mwanzoni mwa wiki ijayo kabla ya kikao na washirika wakuu wa muungano wa Kenya Kwanza.
Soma pia →Kenya: Viongozi watoa wito wa kuvumiliana kisiasa
Inasadikika harakati hizo zitaishia kwa kumteua mgombea mwenza wa muungano huo katika uchaguzi mkuu wa Agosti.Musalia Mudavadi wa chama cha ANC kilicho mshirika mkuu wa Kenya Kwanza anasisitiza kuwa lengo lao ni kuimarisha hali za wakenya.
Kwa upande wake,tume ya uchaguzi na mipaka ya Kenya IEBC imewapa wanaowania urais muda hadi Alhamisi ijayo ambayo ni Aprili 28 kuwa wamewateua wagombea wenza.