Mbunge ataka kifungo wapenzi wa jinsia moja kuondoshwa Ghana
16 Februari 2024Mbunge huyo aliyeshauri adhabu mbadala kujumuisha ushauri nasaha kwa wale watakaotiwa hatiani kwa makosa hayo, alisema muswaada dhidi ya watu hao wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, ambao kwa sasa uko bungeni, utachochea visa zaidi vya ulawiti magerezani.
Afenyo-Markin wa chama tawala cha Ghana alisema siku ya Alhamis (Februari 15) kwamba kufungwa jela kwa watu hao kunafanya hali kuwa mbaya zaidi na kuharibu lengo halisi la muswada huo.
Soma zaidi: Maaskofu Afrika wapinga kuwabariki wapenzi wa jinsia moja
Muswada huo ambao uko katika hatua yake ya mwisho kabla ya kuidhinishwa kuwa sheria, pia unawahimiza wale wanaotuhumiwa kwa kushiriki mapenzi ya jinsia moja kufanyiwa kile kinachofahamika kama "tiba ya kubadili jinsi" inayodaiwa kubadilisha utambulisho wa jinsia, ili nao wapunguziwe vifungo.
Tayari vitendo vya mapenzi ya jinsia moja katika taifa hilo la Afrika Magharibi ni kosa linaloloweza kupelekea adhabu ya hadi miaka mitatu jela kwa anayetiwa hatiani.