1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbio za sakafuni za Mladic zaishia The Hague

1 Juni 2011

Baada ya mbio za miaka 16, hatimaye jenerali wa zamani wa jeshi la Serbia katika Bosnia, Ratko Mladic, amepelekwa The Hague anakotazamiwa kufikishwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita kujibu mashitaka.

https://p.dw.com/p/11SGH
Ratko Mladic
Ratko MladicPicha: AP

Jana usiku (31.05.2011), Ratko Mladic (69) alisafirishwa katika ndege maalum ya serikali ya Serbia hadi Rotterdam, Uholanzi, na kutoka huko alipelekwa jela chini ya ulinzi mkali. Kiasi ya watu 200, hasa waandishi wa habari, walikuwa wakingojea nje ya jela ya Scheveningen ya mjini The Hague.

"Baada ya kuwa mbioni kwa takriban miaka 16, sasa yupo kule tulikotaka kumuona tangu zamani." Alisema msemaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kuhusu Yugoslavia (ICTY), Nerma Jelacic.

Jelacic ameongezea kuwa Mladic atapewa fursa ya kumchagua wakili wake kutoka orodha ya mawakili walioteuliwa na ICTY.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido WesterwellePicha: AP

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, akiwa ziarani nchini Australia, amesema ukweli kuwa Mladic sasa anapaswa kuwajibika mbele ya Mahakama ya Umoja wa Mataifa ni ushahidi imara wa kuongezeka nguvu kwa sheria za kimataifa.

Wakati huo huo, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, amesema huu ni wakati muhimu kwa haki ya kimataifa na kuridhiana katika eneo la Balkan.

"Mawazo yetu na hisia zetu zipo pamoja na wale walioteseka na waliopoteza familia zao wakati wa vita vya iliyokuwa Yugoslavia hasa huko Bosnia na Herzegovina." Amesema Bi Ashton.

Mladic alikamatwa katika kijiji cha Lazarevo, kaskazini mashariki ya Serbia, Alkhamisi iliyopita. ICTY inamtuhumu kuhusika na mauaji ya kimbari, kuwafukuza watu makwao pamoja na uhalifu dhidi ya binadamu.

Vile vile anatuhumiwa kupanga mauaji ya wanaume na vijana 8,000 wa Kiislamu yaliyotokea Srebrenica katika mwaka 1995. Mauaji hayo ni uovu mkubwa kabisa kupata kutokea barani Ulaya tangu kumalizika Vita Vikuu vya Pili.

Wiki hii, Mladic anatazamiwa kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza kujibu mashtaka hayo. Akikataa kuyakubali mashatka hayo, basi atapewa muda siku 30 kufikiria upya na baadaye mahakama, kwa niaba yake, itakanusha mashtaka hayo.

Mwandishi: Andreas Reuter/ZPR
Tafsiri: Prema Martin
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman