1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbinu za kuongeza mavuno Afrika

26 Aprili 2013

Wawekezaji wa kimataifa wanasaka namna ya kuitumia ardhi tupu ya kilimo barani Afrika kwa masilahi yao na yale ya wenyeji wa nchi husika

https://p.dw.com/p/18Nmv
Wakulima wanaotesha viazi vitamu katika shamba moja karibu na Pretoria nchini Afrika kusiniPicha: AFP/Getty Images

Mavuno haba na ardhi kubwa ya kilimo ambayo ni tupu - uwezo wa bara la Afrika katika kuendeleza shughuli za kilimo ni mkubwa. Hata wawekezaji kutoka kila pembe ya dunia wameigundua sekta ya kilimo ya bara la Afrika. Lakini vipi kilimo kitaweza kugeuzwa kuwa cha kimamboleo kwa namna ambayo wakaazi wenyewe wa bara hilo watafaidika na mazingira hayatachafuliwa? Hilo ni suala ambalo wataalamu walilijadili katika kongamano la Wiki ya Biashara ya Afrika, mjini Frankfurt.

Anayetaka kuwekeza katika sekta ya kilimo barani Afrika,anabidi awasaidie pia wakulima wa kienyeji ili waweze kupata mavuno bora na kwa namna hiyo kujiongezea mapato yao. Hayo ni madai ya Mpoko Bokanga wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda, UNIDO.

Anayewajibika ipasavyo anaweza kuchangia kuzuwia mtindo ulioenea wa watu kuyakimbia maeneo ya mashambani, anasema Bwana Mpoko Bokanga:"Watu wanaweza kutumia teknolojia na kurahisisha kazi kwa namna hiyo. Jambo hilo litawavutia zaidi vijana na kuwashawishi wasalie katika maeneo ya mashambani. Na bila ya shaka litasababisha mazao kuongezeka. Faida tupu ndiyo itakayopatikana bila shaka."

Hata hivyo, Mpoko Bokanga anasema teknolojia mpya pekee sio ufumbuzi. Ndio maana UNIDO inatathmini utaratibu mzima wa shughuli za kilimo.Kuanzia kupandisha mbegu mashambani,mavuno,kushughulikiwa hadi kufikia kuuzwa mazao ya mashambani:"Watu inawabidi waangalie wapi zinakutikana dosari,ili waweze kuingilia kati na kuziondowa. Wakijishughulisha na kitu kimoja tu bila ya kujali kwengineko kunatokea nini, basi mali zao walizowekeza hazitoweza kuleta tija ya maana kama ile ambayo ingepatikana kama kila kitu kingeshughulikiwa."

Kampuni ya Amatheon imegundua njia ya maana

Carl Heinrich Bruhn
Carl Heinrich Bruhn,mwenyekiti wa kampuni ya AmatheonPicha: DW

Mmojawapo wa wawekezaji waliodhamiria kufuata shauri hilo ni mjasiriamali wa Kijerumani Carl Heinrich Bruhn, kiongozi wa kampuni ya Amatheon. Kampuni hiyo inataka kuanzisha viwanda vya mazao ya kilimo barani Afrika ili kuweza kuwazidishia mapato wawekezaji wake.

Kwa ajili ya mradi huo wa mwanzo, Carl Heinrich Bruhn amekodi hekari 30 elfu za ardhi nchini Zambia na kwa kipindi cha miaka 99.

Ardhi hiyo ipo katika eneo ambalo kwa muda mrefu lilitengwa kwa ajili ya shughuli za biashara, lakini wenye kumiliki ardhi hiyo hawakuwa na pesa za kutosha kwa ajili ya uwekezaji. Kampuni ya Ametheon imeichunguza vyema hali katika eneo hilo, anasema Bruhn. Kwa sababu Wajerumani hawataki hata kidogo kuingizwa katika kundi moja na wale wanaotajikana kwa "kunyakua ardhi" barani Afrika, yaani kudhibiti ardhi bila ya kuzingatia masilahi ya wenyeji.

Kampuni yake imeshirikiana na jumuia ya wakulima wa Zambia na kubuni mkakati utakaozipatia faida pande zote mbili-anasema Bwana Bruhn. Hadi wakati huu wakulima wanaoishi katika maeneo ya mbali hawakuwa na njia ya kujipatia kwa mfano mbolea,mbegu au madawa ya kuikinga mimea, anasema Cark Heinrich Bruhn:"Kwa kuwa tumedhamiria kuanzisha shamba kubwa, tunaweza kuwapatia vitu hivyo ambavyo wakulima wadogo wadogo wanaweza kuvitumia katika shughuli zao wenyewe za kilimo. Baadaye itafuata hatua ya pili - soko ambalo hadi wakati huu hakuna aliyekuwa na njia ya kufikisha mazao yake sokoni. Njia hiyo tutaianzisha pia kwasababu mazao yatakayopatikana tutayashughulikia na kuyapeleka mji mkuu yakauzwe".

Mwishoni mwa mwezi huu wa Aprili, kampuni ya Amatheon itavuna kwa mara ya kwanza maharagwe yake ya soya. Baadaye wanataka kuotesha ngano. Mazao yote hayo hayajakusudiwa biashara ya nje anasisitiza Bruhn, kwa sababu nchini Zambia kwenyewe mahitaji ni makubwa mno.

Mwandishi: Mösch,Thomas/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Mohammed Khelef