Mbeki akutana na Kiongozi wa upinzani ,Zimbabwe.
4 Julai 2005Johannesburg:
Rais thabo Mbeki wa Afrika kusini amekua na mazungumzo na Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai juu ya kampeni ya kuyabomoa makaazi ya walala hoi inayoendeshwa na serikali ya Rais Robert Mugabe. Msemaji wa Rais Mbeki Bheki Khumalo alisema mazungumzo hayo ya muda wa saa moja yalifanyika jana usiku Ikulu mjini Pretoria. Kampeni hiyo nchini Zimbabwe imewaacha karibu watu laki mbili bila ya makaazi tangu ilipoanza wiki sita zilizopita. Bw Khumalo alisema Rais Mbeki alimuarifu Bw Tsvangirai kwamba amezungumza juu ya suala hilo na Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Kofi Annan ambaye amemteuwa muakilishi maalum kufanya uchunguzi.
Afrika kusini ambayo imekua ikikosolewa kwa kuchukua msimamo laini dhidi ya Mugabe, imesema inasubiri ripoti ya mjumbe huyo wa umoja wa mataifa ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la makaazi la Umoja huo Bibi Annan Tibaijuka, kabla haijachukua hatua.
Rais Mugabe anashikilia kwamba zoezi hilo ni la kupambana na uhalifu, lakini wadadisi wanasema kampeni hiyo ina lenga kuwaadhibu wafuasi wa upinzani.