1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo yakutafuta amani Somalia yaanza tena

31 Mei 2008

-

https://p.dw.com/p/EAOp

MOGADISHU

Mazungumzo yanayofadhiliwa na Umoja wa mataifa ambayo yanatazamiwa kuwaleta pamoja serikali ya mpito ya Somalia na wapinzani wake katika mazungumzo ya ana kwa ana yameanza leo nchini Djibouti.

Duru ya mwanzo ya mazungumzo hayo ambayo wahusika hawakuonana ana kwa ana ilimalizika mwezi Mei tarehe 16 hatua hiyo ilionekana kama ni ushindi mkubwa katika juhudi za kuumaliza mzozo wa Somalia ambao unatajwa na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu na mashirika ya misaada kuyagharimu maisha ya watu elfu sita katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Mazungumzo haya yanafanyika wakati ambapo ujumbe wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa unatarajiwa kutembelea eneo hilo katika ziara yake ya Afrika wiki ijayo.Aidha Umoja wa Afrika umeyatolea mwito makundi yanayozozana kujitolea kwa dhati katika mazungumzo hayo ili kumaliza vita vya muda mrefu nchini Somalia.Kuna wanajeshi 2,600 wa Umoja wa Afrika wanaoweka amani mjini Mogadishu.Somalia imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 1991 baada ya kuangushwa utawala wa rais Muhammed Siad Barre na juhudi chungunzima za kurudisha amani zimeshindwa kufanikiwa.