Mazungumzo yaanza, mapigano yaendelea Sudan kusini
5 Januari 2014Mazungumzo hayo yanayofanyika katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa yana lengo la kumaliza wiki tatu za mapigano ambayo yanahofiwa kuwa yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 1000 katika taifa hilo changa duniani.
"Sudan ya kusini inastahili amani na maendeleo na sio vita," waziri wa mambo ya kigeni wa Ethiopia Tedros Adhanom amesema katika sherehe ya ufunguzi rasmi wa mazungumzo hayo jana Jumamosi(04.01.2014), mazungumzo ambayo yanaweka pamoja ujumbe wa serikali na ule wa kundi la waasi kwa mara ya kwanza.
"Hampaswi kuruhusu vita hivi visivyo na maana kuendelea, mnahitaji kuzuwia vita hivi, na mnahitaji kusitisha vita hivyo leo, na mnaweza," Alisema Waziri Adhanom. Wakati wajumbe wa pande hizo mbili wakiwa wanatabasamu katika hoteli ya kifahari nchini Ethiopia, miripuko mikubwa kutokana na makombora yanayorushwa pamoja na milio ya bunduki za rashasha ilisikika katika wilaya mjini Juba ambako wizara nyingi za serikali , jengo la makao ya rais na bunge yako, amesema mwandishi wa shirika la habari la AFP.
Mapigano yaendelea
Haifahamiki bado nani anahusika na mapigano hayo, ambayo yamemaliza kipindi cha utulivu katika mji huo mkuu. Mzozo huo ulizuka Desemba 15 mwaka jana , ukihusisha vikosi vya jeshi linalomuunga mkono rais salva Kiir dhidi ya wanamgambo watiifu na makamanda wa jeshi walioasi ambao kwa kawaida wanaongozwa na mpinzani wake kisiasa , makamu wa rais wa zamani Riek Machar.
Msemaji wa mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton amekaribisha ufunguzi wa mazungumzo ya amani , wakati huo huo akitoa mwito wa kuachiwa huru kwa viongozi wote wa kisiasa waliokamatwa.
"Tunatoa wito kwa pande zote mbili kujizuwia kutoa matamshi kwa umma ambayo huenda yakachochea wafuasi wao," msemaji huyo ameongeza. Ujumbe wa majadiliano kutoka kila upande umekwisha tumia siku tatu katika mji mkuu wa nchi jirani ya Ethiopia , Addis Ababa. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Ethiopia Dina Mufti amesema mazungumzo kamili rasmi ya ana kwa ana yataanza mchana leo Jumapili.
Amani ni muhimu kwa hali yoyote
"Watu wa Sudan kusini wameteseka katika mapigano ya vita vya ukombozi, na hawatateseka tena katika mikono yetu," amesema Nhial Deng Nhial, mkuu wa ujumbe wa serikali katika majadiliano hayo.
"Tutafanya kila linalowezekana katika kutafuta suluhisho la amani."
Lakini Nhial pia ameonya kuwa "inapaswa kufahamika kuwa" serikali ina "wajibu wa kurejesha amani na usalama katika nchi hiyo kwa njia yoyote ile iliyopo."
Mapigano yamesambaa katika nchi hiyo changa duniani, ambapo waasi wamekamata maeneo kadha katika eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta upande wa kaskazini. Mkuu wa ujumbe wa waasi Taban Deng, gavana wa zamani wa jimbo muhimu la Unity, amesema wana nia ya kufanya mazungumzo ambayo yanaongozwa na kundi la mataifa ya eneo hilo la IGAD. "Tutaendelea kusogea katika kiwango kingine," Deng amesema, ikiwa ni pamoja na majadiliano ya kusitisha mapigano pamoja na "masuala ya kisiasa".
Deng ametaka kuachiwa huru kwa viongozi kadha wa ngazi ya juu wa kisiasa kutoka chama tawala cha Sudan People's Liberation Movement (SPLM), ambao wanashutumiwa kwa kuhusika katika ghasia hizo, ambazo zilianza katika madai ya kufanya mapinduzi.
Wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada wamezidi kutoa onyo kuhusiana na kuongezeka kwa mzozo huo kwa kuwa raia wanaathirika na mzozo katika nchi hiyo ambayo haina bandari yenye wakaazi karibu milioni 11. Jeshi limekuwa likiendelea na mapambano dhidi ya waasi katika juhudi za kuyakomboa maeneo muhimu ya mji wa Bor, mji mkuu wa jimbo la Jonglei, moja kati ya majimbo makubwa nchini humo.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Amina Abubakar