1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Zimbabwe yapiga hatua

16 Oktoba 2008

Mapatano ya kugawana wizara yaweza kufikiwa leo ?

https://p.dw.com/p/Fb9k

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na mpinzani wake Morgan Tsvangirai wa chama cha MDC,wameingia leo katika siku ya tatu ya mazungumzo yao ya kukwamua mvutano ulioibuka kuhusu nyadhifa za mawaziri huku matumaini yakichomoza kuwa muwafaka uko njiani.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, ndie mwenyekiti wa mazungumzo haya yenye shabaha ya kumhimiza rais Mugabe na Tsvangirai kutatua tofauti zao na kugawana madaraka ili kuiokoa Zimbabwe kutoka misukosuko yake ya sasa ya kiuchumi na kisiasa.

"Tumepiga hatua za maendeleo.Tutamaliza mazungumzo kesho"-Rais Mugabe ,aliwaambia hayo maripota hapo jana alipoondoka kwenye mazungumzo.

Mjumbe mkuu wa Tsvangirai,Tendai Biti alisisitiza nae kuwa maenedeleo yamepatikana katika mazungumzo ya jana ya muda wa saa 7.

Akanukuliwa kusema,

"Historia imo kuandikwa na milima inasogea .Ikiwa tutataomba dua sana hii loe kuna kitu kitatokea kesho." Biti aliwaambia jana maripota mjini Harare.

Vyombo vya habari vya Afrika Kusini, vikinukulu duru zisizotajwa, vimeripoti leo kuwa Bw.Tsvangirai amepewa wizara ya fedha -wizara muhimu sana katika nchi iliokumbwa na ughali wa maisha mkubwa mno duniani wa kiasi cha asili-mia milioni 231.

Hii ikabakisha suluhisho : nani anadhibiti wizara ya ndani inayosimamia polisi nchini -vikosi vilivyotuhumiwa na Upinzani nchini Zimbabwe, kutumiwa na chama-tawala cha ZANUPf kuendesha mkomoto na kukanyaga haki za binadamu.

Katika kipindi fulani cha mazungumzo haya, Kiongozi wa MDC Tsvangirai,alitishia kujitoa kwenye mapatano ya muafaka yaliofikiwa hapo kabla kuunda serikali ya Umoja wa Taifa .Hii ilitokana na tangazo la rais Mugabe mwishoni mwa wiki iliopita kwamba atakabidhi wizara muhimu kwa wanachama wake na hivyo angedhibiti yeye barabara jeshi, polisi na vyombo vyengine ya dola vinavyohusika na usalama.

Gazeti la serikali -THE HERALD-limeripoti leo kwamba, yamkini pakatokea mageuzi katika Baraza la mawaziri alilounda Mugabe mwishoni mwa wiki na kuchapishwa katika gazeti la serikali. Mjumbe mwengine wa chama-tawala amesema kuna uwezekano mbali mbali kwa wizara ya fedha kuhusika pia na shughuli za wizara ya ndani na wizara nyengine chache.

Kabla ya mazungumzo haya kuanza, Kiongozi wa Upinzani Tsvangirai ,amesema chama chake cha MDC kinashikilia kugawana madaraka ya nyadhifa za wizara mbili-ulinzi na ya ndani.MDC kimetoa hoja kuwa kinahitaji kudhibiti wizara ya ndani ili kuwahakikishia wafuasi wake hawaandamwi tena kwa mkomoto kama ilivyotokea wakati wa kampeni ya uchaguzi mapema mwaka huu.

Rais wa zamani wa Afrika kusini, Thabo Mbeki alipatanisha mpango wa kugawana madaraka mwezi uliopita pale pande hizo mbili zilipoafikiana kuunda serikali ya Umoja wa Taifa ambamo Mugabe anabakia rais na Tsvingarai, waziri mkuu.

Zimbabwe iliokua mojawapo ya nchi za kiafrika zenye neema ya kiuchumi, kuporomoka uchumi wake kumesababisha ukosefu mkubwa wa chakula huku nusu ya wakaazi wake wakitegemea ruzuku za UM na kiasi cha 80% ya wananachi hawana kazi wala bazi.

Tsvangirai alishinda duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais hapo Machi,mwaka huu lakini alijitoa katika duru ya pili ya uchaguzi huo mwezi Juni akidai matumizi ya nguvu na mkomoto yameua zaidi ya wafuasi wake 100.Umoja wa Ulaya umetishia kuiwekea Zimbabwe vikwazo vipya iwapo mapatano haya hayatatimizwa.Marekani inamtuhumu Mugabe kukiuka muwafaka uliofikiwa.