1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Yemen yakumbwa na wasiwasi

Admin.WagnerD23 Desemba 2015

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mzozo wa Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed, ameonya mchakato wa amani wa Yemen huenda ukavunjika, akisema hakuna uaminifu kati ya pande zinazohasimiana.

https://p.dw.com/p/1HS9j
Ismail Ould Cheikh Ahmed Mjumbe maalum wa umoja wa mataifa
Ismail Ould Cheikh Ahmed Mjumbe maalum wa umoja wa mataifaPicha: picture-alliance/Xinhua/Xu Jinquan/

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mzozo wa Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed, ameonya kuwa mchakato wa amani wa Yemen uko hatarini kuvunjika, akisema hakuna uaminifu kati ya pande zinazohasimiana. Ambia Hirsi anaarifu zaidi.

Akizungumza na wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa, Ould Cheikh Ahmed amesema imebainika kuwa mazungumzo ya amani ya Yemen kati ya serikali inayoungwa mkono na Saudi Arabia na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran, yamegawanyika kwa kiasi kikubwa na pande hizo mbili pia zinatofautiana kuhusu mchakato wa kupatikana amani pamoja na mustkabali wa serikali ijayo.

Mazungumzo ya amani yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kati ya pande hizo mbili nchini Uswisi, yalimalizika bila ya kupatikana muafaka. Mjumbe huyo amesema nchini Yemen kwenyewe, ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano bado unaendelea, hata wakati mashirika ya misaada ya kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa yakionya kuwa raia wanakabiliwa na mashambulizi na wanaishi katika mazingira ya kukata tamaa.

Vikosi vya majeshi ya Saudi Arabia nchini Yemen
Vikosi vya majeshi ya Saudi Arabia nchini YemenPicha: picture-alliance/dpa

Ametoa wito wa kuwepo makubaliano imara na yenye nguvu ya kusitisha mapigano na amezisihi nchi wanachama za Umoja wa Mataifa kuunga mkono juhudi zake za upatanishi kuelekea katika mazungumzo mapya yatakayofanyika mwezi ujao. Amekiri kuna siku ambazo anakuwa na hofu kwamba pande hizo mbili zinaweza kushindwa kutafuta njia ya kukubaliana kuhusu masuala muhimu.

Waasi wa madhebu ya Shia wa Houthi wanamuunga mkono rais wa zamani wa Yemen, Ali Abdullah Saleh wakitaka kuidhibiti serikali, kutoka mikononi mwa vikosi vinavyomtii Rais Abed-Rabbo mansour Hadi. Iran imekuwa ikiwapatia silaha waasi wa Houthi, huku Saudi Arabia ikiungwa mkono na Marekani kusaidia kampeni za muungano wa Waislamu wa madhehebu ya Sunni katika kumuunga mkono Rais Hadi.

Mashirika ya kutoa msaada

Mashirika ya kimataifa yanayofuatialia haki za binaadamu yameushutumu muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kwa kufanya kiholela mashambulizi yanayowalenga raia, huku waasi wa Houthi wakifyatua kiholela makombora.

Kamishna wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al-Hussein ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia unawajibika kwa mashambulizi ya anga dhidi ya makaazi ya raia, shule na hospitali.

Wakati huo huo, mapigano mapya yamezuka Yemen licha ya wito wa Jumuiya ya Kimataifa wa kuweka chini silaha uliokuwa uanze usiku wa kuamkia leo, ambapo waasi 13 wa Houthi wameuawa katika shambulizi la anga kwenye jimbo la Daleh, usiku wa kuamkia leo.

Ama kwa upande mwingine wanamgambo wanne wanaosadikiwa kuwa wapiganaji wa mtandao wa Al-Qaeda, wameuawa katika shambulizi la ndege isiyo na rubani la Marekani.

Afisa wa usalama amesema leo kuwa shambulizi hilo limetokea katikati ya Yemen na lilikuwa linalilenga gari lao karibu na mpaka wa majimbo ya Baida na Shabwa. Aidha, watu wenye silaha wasiojulikana wamemuua kwa kumpiga risasi Kanali Jalal al-Awbali, ambaye pia ni kiongozi wa upinzani wa upande wa kusini kwenye mji wa Aden, usiku wa jana.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE

Mhariri:Iddi Ssessanga