Mazungumzo ya Somalia yagonga mwamba Djibouti
10 Juni 2008Mazungumzo yenye lengo la kuyaleta pamoja makundi yanayohasimiana nchini Somalia yamegonga mwamba.
Mazungumzo hayo ambayo yanadhaminiwa na Umoja wa Mataifa yamekuwa yakiendelea nchini Djibouti.
Kwa mujibu wa afisa mmoja ,anaehudhuria mkutano huo ambae hakutaka jina lake kutajwa, mazunguzo ambayo yalikuwa na lengo la kuyakutanisha pamoja makundi husika na mgogoro wa Somalia yanakumbwa na matatizo kadhaa,lakini hakufafanua zaidi kutokana na hali tete ya mazunguzo hayo.Amesema kuwa japo mazunguzo yanaendelela lakini matumaini ni madogo kufikia muafaka.
Afisa huyo hakuyafafanua matatazo hayo ,lakini habari hizo zinakuja huku kukiwa na taarifa za mji wa Mogadishu kushambuliwa na mizinga kutoka sehemu mbalimbali. Mizinga hiyo, inavurumishwa na wapiganaji wa kiislamu kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine, na vikosi vya Ethiopia vikishirikiana na vya serikali ya Somalia.
Duru hii ya mazunguzo ilianza Mei 31,ikifuatia ya mwanzo iliomalizika Mei 16.
Katika duru ya mwanzo mahasimu hawakukutana ana kwa ana,lakini hatua hiyo ilionekana kama hatua muhimu katika mchakato mzima wa kuumaliza mgogoro ambao pia umeziingiza nchi kadhaa jirani.
Mazungungumzo ya mjini Djibouti,yalipewa msukumo wa aina yake pale ujumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ulipofika huko kujua kile kilichokuwa kinaendelea, Juni 2.
Pia Umoja wa Afrika ambao ulituma kikosi cha kulinda amani mjini Mogadishu,nao umekuwa ukiyaunga mkono mazungumzo hayo.
Huku baadhi ya viongozi wa kiislamu pamoja na wakuu wa koo muhimu wakiwa walikikubali kushiriki katika mazungumzo hayo,lakini vingozi wengine wenye msimamo mkali wameshikilia kuwa upatanishi huo umeegemea upande mmoja na kuzidi kudai kuwa ni lazima vikosi vya Ethiopia viondoke Somalia ili mazungumzo kamili kuweza kuanza.
Ingawa mazungozo ya Djibouti yamekuwa yakiendelea nayo mapambano kati ya wanamgambo wa kiislamu na majeshi ya serikali yamekuwa yakipamba moto.
Mashirika ya kimisaada yanasema kuwa takriban wananchi wa kawaida 6,000 wamefariki kwa kipindi cha mwaka mmoja kutokana na mapigano hayo.
Na hayo yakiarifiwa,eneo hilo la pembe ya Afrika sasa limekumbwa na tatizo lingine mbali na vita. Tatizo hilo ni njaa.
Umoja wa Mataifa unasema kuwa watu zaidi ya millioni 3 katika eneo hilo wanahitaji msaada wa dharura.
Maeneo ambayo yameathirika sana na baa hilo la njaa ni mikoa ya kati na kaskazini ya Ethiopia.
Hali hii imesababisha idadi ya raia wa nchi hiyo wanaohitaji msaada wa dharura kuzidi kupanda kuliko ilivyo kuwa.
Afisa moja wa shirika linaloshughulikia na kuzuia majanga,Simon Mechale amewambia waandishi habari mjini Addis Ababa kuwa,idadi sasa ya watu wanaohitaji chakula imefikia millioni 4 unusu kutoka millioni 2 na ushei
Shirika la kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa la UNICEF, mwezi uliopita lilisema kuwa watu wanaofikia millioni 3 unusu walikuwa wanahitaji msaada wa dharura.
Nayo serikali ya Addis Ababa, hivi majuzi, iliahidi kuwa hakuna tena mtoto wa Ethiopia atakekufa na njaa.
Lakini kuzidi kupanda kwa bei ya vyakula ,kumezidisha hali kuwa mbaya, na hivyo kuifanya serikali kuomba msaada wa dharura kutoka kwa jamii ya kimataifa.