1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya nyuklia yamalizika bila mafanikio

10 Novemba 2013

Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani yameshindwa kufikia makubaliano katika mazungumzo yaliyokusudiwa kupungunza nguvu za programu ya nyuklia ya Iran yaliyokuwa yakifanyika mjini Geneva, Uswisi.

https://p.dw.com/p/1AEo1
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry (wa pili kushoto), Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton (katikati, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif (wa pili kulia) wakihudhuria kikao cha Geneva.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry (wa pili kushoto), Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton (katikati, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif (wa pili kulia) wakihudhuria kikao cha Geneva.Picha: Reuters/Jean-Christophe Bott

Mataifa hayo yamesema, hata hivyo, kwamba tafauti baina yao zimepungua na kwamba watarudi kwenye duru nyengine ya mazungumzo ndani ya siku 10 katika jitihada za kumaliza mkwamo wa muongo mzima kwenye mazungumzo hayo.

Hata hivyo, kumeonekana tafauti za wazi kati ya Marekani na washirika wake wa Ulaya katika siku ya mwisho ya mazungumzo hayo, pale Ufaransa ilipoonesha kwamba mapendekezo yaliyojadiliwa hayakukilainisha kitisho cha Iran kumiliki bomu la nyuklia.

Iran inatarajia makubaliano ambayo yatapekelea kulegezwa kwa vikwazo vya kimataifa dhidi yake ambavyo hadi sasa vimezizuilia mali za nchi hiyo katika mataifa mbalimbali duniai na vinaizuia kuuza mafuta yake.

Wachambuzi wa mambo wanasema kwa hakika hasa ni Iran na Marekani pekee, ambazo hazijawa na mafungamano ya kidiplomasia kwa zaidi ya miongo mitatu, ndizo zenye nguvu za kufikia au kuyavunja makubaliano.

Kerry aona mafanikio na umoja

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alipuuzia uwezekano wa mpasuko miongoni mwa mataifa ya Magharibi, akisema kumekuwa na umoja kwenye dhamira na msimamo wa mataifa hayo.

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif wakihudhuria kikao cha Geneva.
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif wakihudhuria kikao cha Geneva.Picha: Reuters

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, alisema maafisa wa ngazi za juu wa kisiasa kutoka Iran na wajumbe watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani watakutana tena tarehe 20 Novemba kufanyia kazi makubaliano, ambayo Kerry aliwaambia waandishi wa habari yapo karibu kufikiwa.

"Hakuna shaka kwamba sasa tupo karibu sana wakati tukiondoka Geneva kuliko pale tulipokuja na kwamba kwa kazi nzuri na imani njema juu ya jambo hili ndani ya wiki zijazo, kwa hakika tunaweza kufikia lengo letu," alisema Kerry.

"Tulikuja Geneva kupunguza tafauti, na naweza kuwaambieni bila kuongeza chumvi kwamba tumepunguza tafauti na kuziweka bayana zile zilizobakia," alisema.

Lakini akaionya kwamba serikali ya Iran kwamba hamu ya serikali ya Marekani ya kupatikana kwa suluhisho la kidiplomasia kwa mzozo huo wa muda mrefu juu ya programu ya Iran ya nyuklia si wa kudumu, akisema kwamba "mlango wa diplomasia hauwi wazi milele."

Ufaransa yakera wengine

ni siku ya Jumamosi, ghafla makini zilielekezwa kwa Ufaransa baada ya Waziri wa Mambo ya Nje, Laurent Fabius, kuiambia Redio France Inter kwamba nchi yake haitaweza kukubaliana na "mchezo wa kipumbavu" - kwa maana nyengine, makubaliano dhaifu na Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, akihudhuria mkutano wa Geneva.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, akihudhuria mkutano wa Geneva.Picha: Reuters

"Tangu awali, Ufaransa ilitaka makubaliano kwenye suala muhimu la programu ya nyuklia ya Iran," Fabius aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano huo, ambao ulikwenda hadi alfajiri ya Jumapili.

"Mkutano huu wa Geneva ulituwezesha kusonga mbele lakini hatukuweza kufikia suluhisho kwa sababu bado kuna masuala ya kuzungumziwa," alisema Fabius.

Fabius alitoa kauli ambazo ziliyakera mataifa mengine kwenye kambi ya Magharibi. Mwanadiplomasia mmoja aliye karibu na mazungumzo hayo alisema Wafaransa walikuwa wanajaribu kuwapiku wengine na walikuwa wanasababisha usumbufu usio wa lazima kwa washiriki wa mazungumzo hayo, ambayo yalikusudiwa kufikia makubaliano na Iran ambayo imeikwepa Magharibi kwa muongo mzima.

"Wamarekani, Umoja wa Ulaya na Wairani wamekuwa wakishirikiana kwa kiasi kikubwa kwa miezi sasa juu ya pendekezo hili na hiki sio chochote zaidi ya Ufaransa kujiingiza kwenye hatua za mwisho za mazungumzo," mwanadiplomasia huyo aliliambia shirika la habari la Reuters kwa sharti la kutotajwa jina.

Kikao chengine chapangwa

Mawaziri kutoka Iran na mataifa makubwa duniani walikuwa na mkururo wa mikutano hadi jioni sana siku ya Jumamosi kushinikiza ratiba ya makubaliano ambayo yatafunga baadhi ya programu za nyuklia za Iran kwa mabadilishano na kupunguzwa kwa vikwazo dhidi yake. Hata hivyo, hatimaye waliamua kuahirisha kwa siku 10 zaidi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, akihudhuria mkutano wa Geneva.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, akihudhuria mkutano wa Geneva.Picha: picture-alliance/dpa

Ashton na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif, walisema wanatarajia makubaliano yatasainiwa mwishoni mwa mwezi huu. "Tulikuwa na siku tatu nzuri sana, siku tatu zenye manufaa makubwa, na ni kitu tunachoweza kukitegemea," alisema Zarif.

Mazungumzo hayo yalianza siku ya Alhamisi na Kerry aliwasili bila kutarajiwa siku ya Ijumaa kwa kile kilichosema na kusaidia kupunguza tafauti na kutafuta makubaliano. Wakati akiwasili mjini Geneva, Kerry alipuuzia matarajio yoyote ya kufikiwa kwa makubaliano.

Fabius, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza William Hague na wenzao wa Urusi na Ujerumani - Sergei Lavrov na Guido Westerwelle, pia walihudhuria sambamba na Waziri wa Mambo ya Nje ya China, Li Baodong, hatua iliyoashiria utayarifu wa mataifa hayo sita kufikia muafaka.

Hata hivyo, Israel iliyaonya mataifa hayo sita tangu awali kwamba "Iran inaweza ikapata makubaliano ya karne", jambo ambalo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema nchi yake haitakubaliana nalo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Bruce Amani