Mazungumzo ya nyuklia ya Iran yaingia ngazi mpya
18 Februari 2014Mafanikio ya mazungumzo hayo yumkini yakasaidia kuziweka Iran na Marekani katika njia ya kurudisha uhusiano wa nchi hizo mbili katika hali ya kawaida ikiwa ni miaka 35 baada ya mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kuleta tija katika maeneo mengine ikiwemo Syria wakati kushindwa kwake kutapelekea kuzuka kwa mzozo.
Mazungumzo hayo ya siku tatu yanaanza leo mjini Vienna Austria kati ya Iran na mataifa matano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani Uingereza,China,Ufaransa, Urusi na Marekani ikiwemo pia Ujerumani.
Nia ya kisiasa
Waziri wa mambo wa nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema Iran ina nia ya kisiasa kufikia makubaliano kabambe na mataifa hayo makubwa duniani kuhusiana na mpango wake tata wa nuklia
Amekaririwa akisema hyapo jana usiku baada ya kukutana na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton mjini Vienna kwamba wanaamini wanaweza kufikia makubaliano hayo na wamekwenda hapo na nia ya kisiasa kufikia makubaliano ya mwisho.Amesema lengo lao ni kuwasilisha hakikisho katika mazungumzo hayo kwamba wa mpango wa nuklea wa Iran utabakia kuwa kwa ajili ya dhamira za amani.
Amongeza kusema katika taarifa zilizonukuliwa na shirika la habari la serikali nchini Iran IRNA kwamba iwapo pande zote mbili zinaingia kwenye mazungumzo hayo na nia ya kisiasa kulipatia ufumbuzi suala hilo wataweza kupata matokeo mazuri lakini itachukuwa muda.
Matumaini sio makubwa
Kauli yake hiyo inakuja siku moja baada ya Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ambaye ana maamuzi ya mwisho katika masuala muhimu ya taifa.kusema kwamba mazungumzo ya nuklea na mataifa makubwa hayatofika popote lakini hayapingi.
Afisa mwandamizi wa serikali ya Marekani ambaye yuko Vienna kwa ajili ya mazungumzo hayo amesema yumkini wasifikie makubaliano ya kile wanachotaka lakini mazungumzo hayo ni fursa nzuri kuwa kuwa nayo kuiachia diplomasia kutafutia ufumbuzi mojawapo ya changamoto kubwa za usalama za taifa.
Hapo tarehe 24 mwezi wa Novemba mwaka jana mawaziri wa mambo ya nje wa kutoka nchi saba walifikia makubaliano yaliopongezwa kama ya ufumbuzi mkubwa baada ya kushindwa kwa juhudi za kidiplomasia na mvutano wa muongo mzima.
Chini ya makubaliano hayo ambayo yalianza kazi Januari 20 Iran shughuli zake za nuklea kwa kiasi fulani nayo ikaregezewa vikwazo vilioiathiri nchi hiyo pamoja na kuahidiwa kutowekewa vikwazo vipya.
Chini ya makubaliano mapya kabambe ambayo yanajadiliwa hivi sasa na yanayotarajiwa kukamilishwa na kuanza kutekelezwa hapo mwezi wa Novemba Iran itatakiwa kupunguza kabisa shughuli zake za nyuklia au kwamuda mrefu sana.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP
Mwandishi:Mohammed Abdul-Rahman