1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya nyuklia ya Iran yaanza tena

Mohammed Khelef16 Machi 2015

Mazungumzo juu ya nyuklia wa Iran yanaingia wiki yake muhimu mjini Lausanne kwa mkutano kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Marekani kuyakwamua majadiliano ya mwaka mmoja na nusu sasa

https://p.dw.com/p/1ErMT
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry (kushoto), na mwenzake wa Iran, Mohammad Javad Zarif.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry (kushoto), na mwenzake wa Iran, Mohammad Javad Zarif.Picha: Reuters/Brian Snyder

Huku wote wawili wakijuwa kuwa wakati unakwenda mbio haraka, John Kerry na Mohammad Zarif wanatazamia kuanza kuweka utaratibu wa kukamilisha makubaliano hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu, huku mkataba kamili kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani ukitazamiwa tarehe 1 Julai.

Mawaziri hao wa kigeni wa Marekani na Iran walianza mkutano wao saa 1:00 asubuhi, huku wakikabiliwa na shinikizo kali kutoka kwa kambi za wahafidhina ndani ya nchi zao, ambao wanahofia kwamba huenda mawaziri hao wa mambo ya nje wanaweza kuchupa mpaka katika jitihada zao za kuridhishana na hamu yao ya kulifikisha suala lililodumu kwa miongo kadhaa sasa.

Kabla ya kuondoka nchini Misri hapo kuelekea Uswiwi, Kerry aliwatoa wasiwasi wale wenye mashaka na mazungumzo hayo, akisema hayahusu kupatikana kwa makubaliano tu, bali kupatikana kile alichokiita "makubaliano sahihi".

"Ikiwa programu ya nyuklia ya Iran ni ya amani, basi tuiwacheni iwe hivyo na natazamia kuwa ndani ya siku chache zijazo, hilo litawezekana kuwa hivyo." Kerry alikiambia kituo cha televisheni cha CBS, ingawa alikiri kwamba bado kuna maeneo muhimu ambayo pande hizo mbili hazijapata muafaka.

Matumaini ya makubaliano

Kwa upande wake, Zarif alisema kuna masuala kadhaa ambayo yanapaswa kwanza kujadiliwa kwa undani, lakini yapo ambayo kimsingi yalishapatiwa ufumbuzi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, akizungumza na waandishi wa habari juu ya mazungumzo ya Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, akizungumza na waandishi wa habari juu ya mazungumzo ya Iran.Picha: AFP/Getty Images/A. Kenare

Zarif alitazamiwa kwenda mjini Brussels kukutana na wenzake wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, na Umoja wa Ulaya kabla ya kurejea tena Lausanne kuendeleza majadiliano.

Mazungumzo rasmi yanayozishirikisha Urusi, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani yataanza kesho Jumanne, kwa mujibu wa maafisa wa serikali ya Iran.

Marekani na Iran hazina mahusiano ya kibalozi kwa miaka 35, lakini kuchaguliwa kwa Rais Hassan Rouhani hapo mwaka juzi, kulipelekea mabadiliko madogo kwenye mahusiano hayo na pia kutoa msukumo kwenye mzozo huo wa nyuklia.

Kupitia makubaliano ya mpito yaliyofikiwa mwezi Novemba mwaka 2013 kati ya Iran na mataifa hayo sita, Iran ilisitisha utanuzi wa shughuli zake za kinyuklia, huku nayo mataifa hayo yakiondosha sehemu ndogo ya vikwazo vya kiuchumi dhidi yake.

Hata hivyo, kwa maslahi ya Israel, chama cha Republican na washirika wa Marekani kwenye nchi za Ghuba, serikali ya Rais Barack Obama inaonekana kuachana na msisitizo wa kuitaka Iran iachane na shughuli zote za kinyuklia.

Badala yake, inaonekana iko tayari kuvumilia programu ndogo itakayokuwa chini ya uangalizi mkali wa kimataifa na hata kuhamishia baadhi ya vifaa vyake kwenye mataifa mengine, hasa hasa Urusi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman