1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya nyuklia na Iran kuendelea tena wiki ijayo

Sylvia Mwehozi
3 Juni 2021

Wanadiplomasia wa Ulaya wamesema mazungumzo ya hivi karibuni juu ya mpango wa nyuklia wa Iran yamepiga hatua na kuelezea matumaini kwamba makubaliano yanaweza kupatikana siku zijazo kwa Tehran kuheshimu mkataba wa 2015

https://p.dw.com/p/3uNt7
Picha: EU Delegation in Vienna/REUTERS

Afisa wa Umoja wa Ulaya ambaye ameratibu mkutano uliofanyika mjini Viena, Enrique Mora amesema ujumbe kutoka Urusi, China, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Iran na Marekani utarajea nchini mwao kuwasilisha yaliyojitokeza katika mkutano huo kwa serikali na kisha kukutana tena wiki ijayo. Mora amedokeza kwamba ana uhakika mazungumzo ya wiki ijayo yatafikia makubaliano kuhusu suala hilo.

"Ni mchakato mgumu wenye maamuzi ya kisiasa, na masuala ya kiufundi yanaenda sawa. Sasa tumefikia hatua ambayo tunapaswa kukabiliana na maamuzi magumu."

Hata hivyo, wanadiplomasia waandamizi wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, miongoni mwa mataifa yaliyo na nguvu yaliyosaini makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 na Iran walikuwa na tahadhari. Katika taarifa yake, kundi la wanadiplomasia wa mataifa hayo limesema kwamba wanaendelea kupiga hatua na vipengele muhimu katika mkataba wa baadae vimetolewa lakini bado kunatakiwa maamuzi magumu. 

Iran Tehran | Iranischer Präsident | Hassan Rouhani
Rais wa Iran Hassan RouhaniPicha: Iranian Presidency/ZUMA Wire/picture alliance

Wanadiplomasia wengine wawili walisema mazungumzo hayo yaliyoanza mwezi Aprili sasa yako katika awamu ya tano na yatendelea tena kuanzia Juni 10. Lakini ratiba hiyo itakuwa na siku 8 tu kabla ya uchaguzi wa rais wa Iran wa Juni 18 ambao una uwezekano wa kumweka rais mwenye msimamo mkali. Wajumbe wengine wamesema kwamba ingawa kuna uwezekano mkubwa wa makubaliano kupatikana lakini ratiba hiyo inaonekana kuwa na ugumu.

Iran ilianza kuzuia ukaguzi wa mitambo yake ya nyuklia katika jaribio la kushinikiza serikali ya rais Joe Biden wa Marekani kuondoa vikwazo vilivyoanzishwa tena baada ya aliyekuwa rais Donald Trump kujiondoa kwenye makubaliano hayo. Mjini Washington, msemaji wa wizara ya mambo ya nje Jalina Porter aliwaeleza waandishi wa habari kwamba mjumbe wake katika mazungumzo hayo Rob Malley atarajea nchini humo na kupendekeza kwamba mazungumzo yanakwenda polepole.

Naye rais wa Iran Hassan Rouhani alisema kwamba mazungumzo hayo kabla hajaondoka madarakani mwezi Agosti yanahitaji "utashi" nje ya uwezo wake. Rouhani ndiye mratibu mkuu wa makubaliano ya mwaka 2015 na chini yake vikwazo vya kimataifa vililegezwa kwa sharti la Iran kutoendeleza silaha za nyuklia. Lakini uamuzi wa mwisho kuhusu mazungumzo ya Vienna yako mikononi mwa kiongozi mkuu wa taifa hilo la Kiislamu Ayatollah Ali Khamenei.