1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya nyuklia mashariki ya kati yafutwa

24 Novemba 2012

Marekani imesema mazungumzo kuhusu nyuklia katika mashariki ya kati yaliyopangwa kufanyika mwezi ujao hayatafanyika tena, hatua ambayo inaweza kuyakasirisha mataifa ya Kiarabu lakini ikaifurahisha Israel.

https://p.dw.com/p/16p7q
Bendera za Iran zikipepea katika moja ya vituo vya nyuklia vya nchi hiyo.
Bendera za Iran zikipepea katika moja ya vituo vya nyuklia vya nchi hiyo.Picha: dapd

Sababu za kufutwa kwa mkutano

Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani ilitangaza kuwa mkutano huo uliyokuwa imepangwa kufanyika katikati ya Desemba wenye lengo la kuanzisha ukanda huru dhidi ya silaha za maangamizi, na taarifa yake haikuweka wazi ni lini au kama utafanyika tena. Mwanzoni mwa mwezi huu wanadiplomasia waliliambia shirika la habari la Reuters kwamba mazungumzo hayo yalikuwa na uwezekano wa kusogezwa mbele kuliko kuyafuta kabisa.

Msemaji wa wizara ya mabo ya kigeni ya Marekani, Victoria Nuland.
Msemaji wa wizara ya mabo ya kigeni ya Marekani, Victoria Nuland.Picha: AP

"Kama mdhamini mwenza wa mkutano huo, Marekani inasikitika kutangaza kuwa mkutano hauwezi kufanyika kwa sababu ya hali inayoendelea mashariki ya kati, na ukweli kwamba mataifa hayajafikia makubaliano juu ya masharti yanayokubalika kwa ajili ya mkutano huo," alisema msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Nuland alisema kuna tofauti kubwa miongoni mwa mataifa juu ya namna ya kushughulikia usalama wa kanda na udhibiti wa silaha, na kuongeza kuwa mataifa ya nje hayawezi kulaazimisha mchakato huo zaidi ya yanavyoweza kulaazimisha matokeo. Mpango wa mkutano wa kuweka mikakati ya uwezekano wa kuanzisha kanda isiyo na silaha za maangamizi ulikubaliwa wakati wa mkutano mwezi Mei 2010, wa wadau 189 wa mkataba wa kuzuia ueneaji wa silaha za nyuklia wa mwaka 1970, NPT.

Hofu ya Marekani

Marekani ilihofia kwamba mkutano huo ambao ulikuwa ufanyike nchini Finnland, ungetumika kama jukwaa la kuishambulia Israel, wasi wasi ambao unaonekana kuongezeka baada ya siku nane za mapigano makali baina ya Israel na Hamas yaliyomalizika kwa makubaliano ya siku ya Jumatano. Iran na mataifa mengine ya kiarabu yanasema malimbikizo ya silaha za nyuklia ya Israel yanatishia usalama na amani katika eneo hilo. Israel na mataifa ya magharibi wanaiona Iran kama tishio kubwa kutokana na mipango yake ya nyuklia. Iran inakanusha madai hayo.

Mfumo wa kuzuia makombora wa Israel ukifanyiwa majaribio.
Mfumo wa kuzuia makombora wa Israel ukifanyiwa majaribio.Picha: AP

Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani ilisema itaendelea kufanya kazi kujaribu kufanikisha mkutano huo, na kuongeza kuwa mkusanyiko kama huo laazima uzingatie usalama wa mataifa yote katika kanda na kuendeshwa kwa misingi ya maafikiano, na hivyo kuihakikishia Israel na wengine wote, kura ya turufu. "Hatutaki kuwa na mkutano ambapo nchi moja itashinikizwa na kutengwa," alisema Nuland, katika hatua ya wazi inayoonyesha wasi wasi wa Marekani kwamba Israel itakamiwa na washiriki wa mkutano huo.

Matumaini bado ni madogo sana

Marekani na Israel zimesema kuwa kanda huru dhidi ya silaha za nyuklia katika kanda ya mashariki ya kati haitawezekana hadi kuwepo na amani ya kudumu baina ya mataifa ya kiarabu na Isreal, na Iran isitishe mpango wake wa nyuklia. Kama nchi za Pakistan na India zenye silaha za nyuklia, Israel haija saini mkataba wa NPT. Haikubali wala kukanusha kuwa silaha za nyuklia, ingawa wachambuzi wa uzuiaji wa kuenea silaha za nyuklia na wale wa usalama wanaamini inamiliki mamia ya silaha za atomiki.

Kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei na rais wa nchi hiyo Mahmoud Ahmadnejad.
Kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei na rais wa nchi hiyo Mahmoud Ahmadnejad.Picha: AP

Hata kama mazungumzo hayo yatafanyika, wanadiplomasia wa mahagribi hawatarajii kuwepo na maendeleo ya kuridhisha katika muda mfupi kutokana na uhasama uliyoota mizizi katika kkanda hiyo, hususani mgogoro wa Israel na mataifa ya kiarabu, na wasi wasi wa Israel juu ya mpango wa iran wa nyuklia. Taifa hilo la Kiislamu liko katika msuguano na mataifa makubwa ambayo yanalishuku kuwa linataka kutengeneza silaha za nyuklia. Israel haijaondoa uwezekano wa kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Sekione Kitojo