Mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Iran yaendelea
10 Novemba 2014Mazungumzo hayo ambayo leo yameingia siku yake ya pili kikao ambacho hakikuwa kimepangwa, yanawakutanisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry na mwenzake wa Iran, Mohammad Javad Zarif, pamoja na mjumbe wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton.
Wanadiplomasia hao wanaendelea na juhudi za kuutatua mzozo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran uliodumu kwa muongo mmoja kati ya Iran na mataifa ya Magharibi, hatua inayozusha wasiwasi wa kuwepo mzozo mkubwa katika Mashariki ya Kati.
Mazungumzo hayo yanafanyika kabla ya kufikiwa tarehe 24 Novemba mwaka huu, ambayo ni tarehe ya mwisho iliyopangwa ya kukamilisha mazungumzo hayo na kufikiwa kwa mpango wa nyuklia. Jana Jumapili (09.11.2014), Kerry, Zarif na Ashton walikuwa na mazungumzo yaliyodumu kwa zaidi ya saa 5. Hata hivyo, mkutano huo ulikuwa wa siri na wanadiplomasia hao hawakutoa maelezo yoyote kwa waandishi wa habari.
Wanadiplomasia wakiri bado kuna tofauti kubwa
Aidha, wanadiplomasia hao wote wamekiri kuwa bado kuna tofauti kubwa katika misimamo ya mazungumzo hayo na kufikiwa kwa mpango wa nyuklia ambao unaitaka Iran kupunguza matumizi yake ya nyuklia na mataifa ya Magharibi kupunguza vikwazo dhidi ya Iran.
Huku Iran na Marekani zote zikikabiliwa na shinikizo la ndani, Rais Barack Obama wa Marekani, amesema pande hizo mbili bado ziko mbali katika kufikia makubaliano. Hata hivyo, kabla ya mkutano huo, Zarif alisema iwapo upande wa pili utaonyesha dhamira yake njema katika upande wa kisiasa, basi makubaliano yanaweza kufikiwa.
Zarif alisema, ''lakini nadhani masuala muhimu yanayopaswa kujadiliwa ni kuhusu kurutubisha madini ya urani na vikwazo. Ni muhimu kwa nchi za Magharibi kuelewa kwamba vikwazo kamwe haviwezi kuchangia katika kupata suluhisho la suala hili. Alifafanua kuwa vikwazo siyo sehemu ya suluhisho, vikwazo ni zaidi ya sehemu ya tatizo, kiasili vikwazo siyo halali, lazima viondolewe kwa sababu havijaleta matokeo yoyote mazuri.''
Serikali ya Iran inaendelea kushikilia msimamo wake kwamba mpango wake huo wa nyuklia unaotiliwa mashaka na mataifa ya Magharibi ni kwa ajili ya matumizi ya kiraia na kisayansi. Mbali na Ashton, Kerry na Zarif, wapatanishi wa mazungumzo hayo kutoka Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani na Urusi, wanatarajiwa kuhudhuria awamu ya mwisho ya mazungumzo hayo yatakayofanyika mjini Vienna, tarehe 18 Novemba, mwaka huu.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFP,AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman