Mazungumzo ya Lebanon na Israel yamekuwa na tija
14 Oktoba 2020Marekani na Umoja wa Mataifa zimesema kuwa Lebanon na Israel zimefanya mazungumzo yenye tija kuhusu mpaka wa bahari unaozozaniwa.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani na ofisi ya mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, imeeleza kuwa wawakilishi wa mkutano huo walionesha nia ya kujitolea zaidi kuendelea na mazungumzo baadae mwezi huu. Mazungumzo mapya yamepangwa kufanyika Oktoba 28.
Marekani na Umoja wa Mataifa ambazo zimekuwa zikisaidia kuwa wapatanishi katika mzozo huo wa muda mrefu, zimesema kuwa mazungumzo ya Jumatano yaliyodumu chini ya saa moja, yamefanyika kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa katika mji wa mpaka wa Lebanon wa Naqoura, chini ya mwenyeji wake Jan Kubis na mbele ya ujumbe wa Marekani, ukiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayehusika na masuala ya Mashariki, David Schenker na Balozi wa Marekani nchini Algeria, John Desrocher.
Makubaliano ya kufanyika mazungumzo hayo yalitangazwa wiki kadhaa baada ya Marekani kuingilia kati kuwashinikiza washirika wa kundi la Hezbollah nchini Lebanon linaloungwa mkono na Iran, kuweka vikwazo kwa mwanasiasa wa ngazi ya juu kutoka kwa mshirika wake mkuu wa madhehebu ya Kishia, chama cha Amal.
Kundi la Hezbollah, ambalo lilipigana vita vya mwezi mmoja na Israel mwaka 2006, limesema mazungumzo hayo sio ishara yoyote ya kufikiwa kwa amani na Israel, wala kurejesha uhusiano na hasimu wake huyo wa muda mrefu.
Ujumbe wa Israel uliokuwa na watu sita, umeongozwa na Udi Adiri, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Nishati. Waziri wa Nishati wa Israel, Yuval Steinitz amesema ujumbe wa Israel utaendelea na mazungumzo hayo ili kutoa nafasi kwa mchakato.
Naye mkuu wa Ujumbe wa watu wanne kutoka Lebanon, Brigedia Jenerali Bassam Yassin amesema mkutano wa leo ni wa kiufundi na uanwakilisha hatua ya kwanza katika safari ya maili elfu moja ya kuweka mipaka ya kusini. Afisa huyo wa ngazi ya juu wa kijeshi amesema wanatarajia kulifikia lengo lao ndani ya muda muafaka. Nazipongeza juhudi za Marekani ambazo zilisaidia kuanzisha mazingira mazuri na ya kujenga wakati wa mazungumzo haya,'' alifafanua Brigedia Jenerali Yassin
Hata hivyo, chombo cha habari cha Lebanon, MTV kiliripoti kuwa ujumbe kutoka pande zote ulikaa mbele ya kila mmoja, lakini hawakuweza kuzungumza moja kwa moja. Kwa mujibu wa duru za serikali ya Lebanon ambazo hazikutaka kutajwa majina yao, hatua hiyo ilikuwa ni ''mkutano wa kiitifaki.'' Jana, Rais wa Lebanon, Michel Aoun aliyaita mazungumzo hayo kuwa ya kiufundi.
(AP, AFP, DPA, Reuters)