Makubaliano yasipofikiwa uchaguzi mpya huenda ukaitishwa
17 Novemba 2017Wawakilishi wa vyama ndugu vya kihafidhina vya Kansela Merkel Christian Democratic Union CDU na Christian Social Union CSU, chama cha Free democratic Party FDP na kile cha walinzi wa mazingira die Grüne waliwaambia waandishi habari leo saa kumi alfajiri kwamba wanapumzika baada ya masaa 15 ya majadiliano ya kukatisha tamaa, na wanatarajia kurejea katika vikao vyao baadaye leo mchana.
"Bado tunaamini kwamba tunapaswa kulifanyia kazi hili kwa nguvu zetu zote, lakini kwa upande mwengine ni wazi kwamba ni ngumu," alisema Peter Tauber, Katibu mkuu wa chama cha Kansela Merkel cha CDU.
Wolfgang Kubicki, Naibu kiongozi wa chama cha FDP aliwaambia waandishi habari kuwa ameghadhabishwa na kukatishwa tamaa baada ya wiki nne za majadiliano yaliyoshindwa kufikia makubaliano ya pamoja.
Amesema iwapo hali itaendelea kama ilivyo kwa sasa majadiliano hayatafika kokote, ameongeza kuwa inasikitisha kukaa pamoja katika majadiliano lakini baadaye unatambua mnarejea pale pale mlipoanzia bila ya mafanikio.
Kwa upande wake Kiongozi wa CSU Horst Seehofer amesema masuala ya uhamiaji pamoja na mambo mengine ndiyo yanayokwamisha majadiliano hayo.
"Ni muhimu sana kwetu kwamba Uhamiaji hautaongezeka, idadi tuliyonayo kwa sasa pamoja na kuunganishwa kwa familia ni kubwa mno na ndio maana hatuwezi kufikia suluhu itakayopelekea ongezeko la wahamiaji," alisema Seehofer.
Iwapo makubaliano hayatafikiwa basi uchaguzi mpya huenda ukaitishwa.
Masuala ambayo bado ni changamoto kubwa katika meza ya mazungumzo ni suala la hifadhi ya wakimbizi uhamiaji na kuungana kwa familia, ulinzi wa mazingira, fedha, usalama wa ndani, pamoja na Umoja wa Ulaya na sera ya sarafu katika kanda ya euro. Hata hivyo Michael Kellner, afisaa mkuu katika chama cha walinzi wa mazingira cha kijani amesema bado kuna kazi kubwa ya kufanywa hakuna kilichokubaliwa na hakuna pia kilichoamuliwa.
Muakilishi mwengine kutoka chama cha kijani amesema kuna hatua zilizopigwa juu ya kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya nishati yanayotokana na makaa ya mawe lakini chama ndugu cha kihafidhina cha Bavaria CSU kimekataa kukubaliana juu ya suala la wahamiaji wanaotaka hifadhi waliyotaka kuleta familia zao haraka iwezekanavyo nchini Ujerumani.
Aidha Merkel alitaka majadiliano haya ya kutathimini uwezekano wa kuundwa serikali ya mseto kukamilika siku ya alhamisi lakini hilo halikuwezekana kufuatia changamoto iliyoko ya kufikia makubaliano.
Hata hivyo kushindwa kufikia makubaliano juu ya Muunganao wa Jamaica jina linalotokana na rangi ya vyama hivyo kufanana na bendera ya Jamaica huenda ikasababisha Ujerumani kurejea tena debeni na kuandaa uchaguzi mpya.
Mwandishi: Amina Abubakar AP/AFP/dpa
Mhariri: Yusuf Saumu