1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Korea Kaskazini na China yatiwa kiwingu

Admin.WagnerD21 Juni 2017

Kifo cha  Mmarekani Otto Wambier baada ya kurudi kutoka kifungoni Korea Kaskazini kinaendelea kuzusha hasira kwa serikali ya Marekani na kutishia kutia kiwingu mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya Marekani na China.

https://p.dw.com/p/2f83l
USA China Donald Trump und Xi Jinping
Picha: Picture alliance/Photoshot/L. Hongguang

Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akiitegemea China kutumia karata yake ya kiuchumi katika kukabiliana na serikali ya kidikteta ya Korea Kaskazini ya Kim Jong Un wakati wasi wasi wa Marekani ukizidi kuongezeka kutokana na kuendelea kwa juhudi za Korea Kaskazini kumiliki kombora litakalowekwa kichwa cha silaha za nyuklia ambalo linaweza kupiga ardhi ya Marekani.

Wanadiplomasia wa ngazi ya juu na wakuu wa ulinzi wa Marekani na Korea Kaskazini wanakutana katika mji mkuu wa Marekani kwa ajili ya mazungumzo ya usalama na Korea Kaskazini litakuwa kipau mbele kwa mujibu wa Susan Thorton ambaye ni mwanadiplomasia mwandamizi wa Marekani kwa Asia mashariki.Mataifa hayo yenye nguvu duniani yanajaribu kujenga msukumo chanya ulioanzishwa wakati Trump na Rais Xi Jinping wa China walipokutana huko Florida hapo mwezi wa April.

Majadiliano hayo yanachukuwa nafasi ya mkakati mpana na mazungumzo ya kiuchumi yaliokuwa yakifanyika kila mwaka chini ya utawala wa Obama. Ni mara chache hutowa matokeo ya maana.Mazungumzo ya mwaka huu yanayatenganisha masuala ya usalama na Waziri wa mambo ya nje Rex Tillerson na Waziri wa ulinzi Jim Mattis watakuwa wenyeji wa mkuu wa sera za kigeni wa China Yang Jiechi na Generali Fang Fenghui mkuu wa idara ya majeshi yote ya Jeshi la Ukombozi la China.

Kitakachozungumziwa

USa Washington - Susan Thornton
Susan Thorston mwanadiplomasia mwandamizi wa Marekani.Picha: picture-alliance/Photoshot/B. Dandan

Thorton amesema mazungumzo hayo yatahusu Bahari ya China Kusini, ambapo ujenzi wa visiwa unaofanywa na China na ujenzi unaoweza kuwa wa vituo vya kijeshi kumewakasirisha nchi jirani na kusababisha mvutano na serikali ya Marekani,ushirikiano wa kijeshi kati ya Marekani na China kupunguza hatari ya mzozo na juhudi za kulishinda kundi linalojiita Dola la Kiislam.Masuala ya biashara yanayoleta mgawanyiko pia yatashughulikiwa katika nyakati tafauti huko mbele.

Wakati Trump amemwagia sifa Rais Xi kwa kujaribu kuidhibiti Korea Kaskazini ambayo inaitegemea China kwa asilimia 90 ya biashara yake juhudi hizo hazikuzaa matunda makubwa.Trump inaonekana kukiri hayo kwa kiasi kikubwa katika mtandao wa Twitter leo hii ikiwa ni siku moja baada ya kifo cha Warmbier.

Trump amendika " Wakati nathamini sana juhudi za Rais Xi na China kusaidia katika suala la Korea Kaskazini hazikufanikiwa.Angalau ninachokijuwa China imejaribu!"

Mchango wa China ni mkubwa

Nordkorea US-Student Otto Warmbier in Pjöngjang
Marehemu Otto Warmbie wakati akishikiliwa Korea Kaskazini.Picha: picture-alliance/Photoshot

Kufuatia kauli hiyo ya Trump China imesema Jumatano(21.06.2017) imefanya juhudi kubwa kutatuwa mvutano katika rasi ya Korea. Geng Shuang ni msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China amesema

" China imefanya juhudi kubwa kulitatuwa suala la nyuklia la Korea na daima imekuwa ikionyesha kwamba imekuwa ni muhimu na inatumika kwa tija.Kujumlisha kila mwenye macho anaweza kuona mchango wa China na taathira ya China inahitajika."

Haijulikani sababu ya kifo cha Wambier mwenye umri wa miaka 22 ambaye alikuwa akishikiliwa kwa takriban mwaka mmoja na nusu nchini Korea Kaskazini kabla ya kurudishwa nyumbani akiwa hana fahamu wiki iliopita.Mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Virginia alikuwa akituhumiwa kwa kujaribu kuiba bango la propaganda wakati akiwa ziarani na kundi lake la utalii na alipatikana na hatia ya kutaka kupinduwa serikali. Familia yake inailaumu Korea Kaskazini kwa vitendo vya mateso ya kikatili.

Kuanzia bunge hadi Ikulu ya Marekani shinikizo limekuwa likizidi kuongezeka kwa Marekani kuchukuwa hatua kali. 

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman