Mazungumzo ya hali ya hewa uaminifu unakosekana , Merkel
3 Mei 2010Kansela wa Ujerumani Angela Merkel jana aliwataka mawaziri wa mazingira kutoka duniani kote kutafuta msingi kwa ajili ya uaminifu, kabla ya mkutano ujao wa umoja wa mataifa mjini Cancun, akikumbushia mkutano wa Copenhagen wa hali ya hewa ambao nusura uvunjike.
Alikuwa akifungua mkutano wa siku tatu mjini Bonn unaoangalia njia za kufufua mazungumzo ya hali ya hewa baada ya mkutano wa Copenhagen kushindwa kufikia makubaliano.
Merkel amesema kuwa kitu kimoja ambacho hakikuweza kufanyakazi mjini Copenhagen ni kwamba kundi dogo lilikutana na makundi ya kimkoa yalijihisi kuachwa kando ya mjadala. Amesema hayo wakati wajumbe kutoka mataifa 45 wakijikusanya ili kuweza kuyapa uhai mpya mazungumzo yaliyokwama ya hali ya hewa.
Kazi ya matayarisho kabla ya mkutano wa Cancun itakuwa kutafuta msingi wa kuleta hali ya kuaminiana kwa mataifa ambayo yatakuwapo katika mji wa Cancun ili kwamba hakuna kundi litakalojihisi kuwa limeachwa nje, Merkel amewaambia mawaziri na wajumbe wa majadiliano.
Kwa upande mmoja tunafungwa na lengo letu la kupatikana makubaliano. Lakini kwa upande mwingine haitakuwa na maana, kwa muda wote kujadiliana kuhusu nadharia, na kusababisha jazba na mivutano mwaka hadi mwaka bila ya kuwa na kitu chochote cha kuanzia.
Mengi ya mataifa 194 yaliyomo katika mfumo wa mkataba kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, UNFCCC hayajaunga mkono mkataba wa Copenhagen, yakilalamika kuwa umefikiwa katika dakika za mwisho kwa faragha na nchi chache zenye nguvu za kiuchumi zikiongozwa na China na Marekani.
Mkataba huo unaopingwa unataka kupunguzwa kwa gesi zinazoharibu mazingira kwa kiasi kinachotosha ili kubakisha hali ya ujoto kutopanda kwa zaidi ya nyuzi joto 2.0 Celsius, lakini hautoi nafasi ya kugawana majukumu ya kufikiwa lengo hilo.
Mkutano huo wa siku mbili unusu , ambao ni mkutano wa ngazi ya juu wa hali ya hewa tangu ule wa mwezi Desemba uliozua mivutano, ulifunguliwa kwa pamoja na rais wa Mexico Felipe Calderon ambaye atakuwa mwenyeji wa mkutano wa Cancun utakaofanyika Novemba mwaka huu , na kansela Merkel.
Calderon pia amesisitiza haja ya kujenga hali ya kuaminiana , hususan katika suala la kuzipatia fedha nchi masikini ambazo zinapambana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Mkuu wa mkutano wa umoja wa mataifa kuhusu hali ya hewa Yvo de Boer ameeleza matumaini yake leo Jumatatu kuwa majadiliano yaliyokwama ya mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kuanza tena, licha ya kushindwa mwaka jana katika mkutano wa Copenhagen.
De Boer amesema katika mkutano huo usio rasmi mjini Bonn kuwa nia ni kubuni miundo mbinu inayofanyakazi kuhusiana na mkutano ujao wa hali ya hewa.
Mwandishi: Sekione Kitojo/ DPAE/AFPE
Mpitiaji: OummilKheir Hamidou