1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya dharura yafanyika Uhispania

Mjahida3 Juni 2014

Waziri Mkuu wa Uhispania, Mariano Rajoy anafanya mazungumzo ya dharura na baraza lake la mawaziri kutengeneza njia halali ya kujiuzulu kwa mfalme Juan Carlos na nafasi yake kuchukuliwa na mwanawe Felipe

https://p.dw.com/p/1CBOB
Raia wa Uhispania wakipeperusha bendera ya nchi hiyo
Raia wa Uhispania wakipeperusha bendera ya nchi hiyoPicha: Reuters

Ubadilishanaji huo wa madaraka hauwezi kufanyika mpaka serikali ya Uhispania itakapoandaa mfumo wa namna Mfalme Carlos atakavyoachia madaraka na jinsi mwanawe atakavyochukua uongozi. Mpango huo hata hivyo tayari umeshakubaliwa bungeni na kwa sasa unasubiriwa kupitishwa kuwa sheria.

Mfalme Juan Carlos aliye na umri wa miaka 76 na mwanawe Felipe aliye na umri wa miaka 46 walionekana katika sherehe za kijeshi hii leo mjini Madrid wakati Rajoy alipokuwa anakutana na baraza lake la mawaziri.

Mfalme Carlos aliongoza kipindi cha mpito nchini Uhispania kutoka katika utawala wa kidikteta hadi katika utawala wa kidemokrasia, lakini akakumbwa na visa vilivyomuharibia sifa hasa wakati Uhispania ilipokuwa inapitia kipindi kigumu cha matatizo ya kifedha.

Waziri Mkuu Mariano Rajoy
Waziri Mkuu Mariano RajoyPicha: Getty Images

Mfalme huyo alitangaza hapo jana kwamba anajiuzulu kwasababu mwanawe yuko tayari kuchukua madaraka na kwamba Uhispania inahitaji ukurasa mpya wa matumaini.

Hata hivyo, tangu tangazo hilo, maelfu ya waandamanaji wamejitokeza mitaani kutaka kwanza Wahispania waulizwe ikiwa bado wangelipendelea kuendelea na ufalme. Lakini Waziri Mkuu Mariano Rajoy ameonya kuwa huenda hatua hiyo ikahitaji katiba ya nchi hiyo kufanyiwa mabadiliko.

"Uhispania ni nchi ya kidemokrasia, na kwa nchi iliyo na demokrasia, sheria ni kitu muhimu sana. Sasa hivi tunaona watu wakitaka kufanyika kura ya maoni, wengine wakitaka mabadiliko, na wengine wakitaka mambo mengine. Mtu yeyote anayetaka kubadilisha namna mchezo unavyokwenda anaweza kufanya hivyo, lakini wanapaswa kutumia mambo yaliopitishwa kisheria kwa kupendekeza marekebisho ya katiba mahakamani," Alisema Mariano Rajoy.

Maandamano ya kupinga utawala wa kifalme yafanyika

Saa kadhaa baada ya Mfalme Juan Carlos kutangaza kujiuzulu hapo jana, maelfu ya watu walikusanyika katika uwanja mkuu wa mjini Madrid wa Puerta del Sol kupinga uwepo wa utawala wa kifalme nchini Uhispania.

Mfalme Juan Carlos na mwanawe Felipe
Mfalme Juan Carlos na mwanawe FelipePicha: Reuters

Hata hivyo maoni ya warepublikan yanabakia kujulikana na wengi katika nchi hiyo ilioanza utawala huo wa kifalme mwaka wa 1975, baada ya kifo cha Jenerali Francisco Franco, aliyeiongoza Uhispania kwa takriban miongo minne.

Kupingwa kwa utawala huo wa kifalme nchini Uhispania ulianza wakati wahispania walipokasirishwa na safari ya kuwinda tembo iliofanywa na mfalme Carlos mwaka wa 2012 nchini Botwana katika kipindi ambacho raia wa nchi hiyo walipokuwa wakingangana kupata kazi wakati uchumi wa nchi hiyo ulipokuwa unayumba.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef