1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Amani ya Mashariki ya Kati Yakwama

25 Aprili 2014

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry anasema Marekani haiko tayari kufutilia mbali mazungumzo ya amani ya Mashariki ya kati hata baada ya Israel kuvunja mazungumzo pamoja na viongozi wa Palastina.

https://p.dw.com/p/1BoMB
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na baraza lake la mawaziriPicha: picture-alliance/dpa

"Daima kunaibuka uwezekano wa kusonga mbele." anasema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani.Hata hivyo John Kerry anahisi waisrael na wapalastina wanabidi wafikie maridhiano ili mazungumzo yaliyoanza miezi tisa iliyopita yaweze kuendelea baada ya April 29 ijayo-wakishindwa anasema na hapa tunanukuu" basi amani haitakua rahisi kupatikana".

"Kamwe hatutakata tamaa au kuachilia mbali jukumu letu la kusaka amani" ameshadidia waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani.

Maamuzi kadhaa yamepitishwa katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita na pande zote mbili ,Israel na Palastinaa na kuzidi kukorofisha mazungumzo ya amani ambayo tokea hapo ni tete .

Serikali ya Suluhu ya Wapalastina ndio Mzizi wa Fitina

Msemaji wa wizara hiyo Jen Psaki amesema John Kerry amezungumza na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas na kumuelezea msimamo wake dhidi ya mipango ya kuundwa serikali ya suluhu pamoja na Hamas-wanaotajwa na Marekani ,Umoja wa Ulaya na wengineo kuwa ni magaidi.

Einigung zwischen Fatah und Hamas April 2014
Wapalastina wanasherehekea suluhu Kati ya Fatah na HamasPicha: DW/K. Shuttleworth

Hapo awali waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema"kamwe hatojadiliana na serikali ya Palastina inayowajumuisha watu wanaotoa wito wa kuteketezwa Israel."Benjamin Netanyahu anamtuhumu Mahmoud Abbas kuwatanguliza mbele Hamas badala ya amani."

Hata hivyo mkuu wa tume ya Israel katika mazungumzo ya amani bibi Tzipi Livni ambae ni waziri wa sheria wa Israel ameelezea matumaini yake kuona ufumbuzi unapatikana ili mazungumzo yaendelee.

Duru mpya ya mazungumzo ya amani iliyoanza msimu wa kiangazi mwaka jana,ilikuwa imalizike April 29 ijayo kwa kupatikana makubaliano ya kuundwa madola mawili.

Marekani haijakata Tamaa

Tangu wakati huo hakuna makubwa yaliyofikiwa na wanadiplomasia walikuwa wakijitahidi kutafuta ridhaa ili mazungumzo yaendelee kwa miezi kadhaa mengine baada ya April 29.

Kerry in Israel Benjamin Netanjahu 31.03.2014
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry (kulia) na waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Reuters

Haijulikani bado kwa muda gani Marekani inapanga kuachilia kizungumkuti hiki kiendelee.Kilichodhahir na kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani, Jen Psaki , wapatanishi wa Marekani watasalia angalao kwa sasa katika eneo hilo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman