1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo mapya kuhusu silaha za kinyuklia za Korea Kaskazini

Maja Dreyer8 Februari 2007

Miezi minne baada ya Korea Kaskazini kutekeleza majaribio yake ya kwanza ya mabomu ya kinyuklia, kunafanyika mkutano mwingine wa kujadiliana juu ya Korea Kaskazini kuacha silaha zake za kinyuklia.

https://p.dw.com/p/CHKW
Kwenye mkutano uliopita kuhusu Korea Kaskazini mjini Beijing
Kwenye mkutano uliopita kuhusu Korea Kaskazini mjini BeijingPicha: AP

Mazungumzo juu ya kumalizika mradi wa silaha za kinyuklia wa Korea Kaskazini yalifunguliwa rasmi mjini Beijing leo hii, wakati Uchina mwenyeji wa wajumbe kutoka nchi sita iliacha wazi muda na mada za mazungumzo hayo.

Alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Beijing, mjumbe wa Korea Kaskazini, Kim Kye Gwan, amesema nchi yake iko tayari kuanzisha upya mazungumzo juu ya mradi wake wa kinyuklia, lakini kuongeza kuwa mafanikio yoyote yanaitegemea Marekani kuachana na sera zake za uhasama kuelekea Korea Kazkasini. Bw. Kim amesema, na hapa tunamnukuu: “Tunapanga kupambanua iwapo Marekani itabatilisha sera zake za kiadui dhidi yetu na kukaribia kuishi pamoja kwa amani au la.” - mwisho wa kumnukuu mjumbe wa Korea Kaskazini Kim Kye Gwan.

Bw. Kim pia amesema kuwa atazumgumzia hatua za kwanza za kutekeleza kauli ya pamoja juu ya kanuni za kumaliza mradi wa kinyuklia ambayo imeafikiana na nchi hizo sita mnamo mwezi wa Septemba mwaka 2005.

Mwakilishi maalum Marekani katika mazungumzo haya, Bw. Christoph Hill, pia alitaja maafikiano hayo ya mwaka 2005 kuwa ni msingi wa mkutano huu wa Beijing.

Katika maafikiano hayo ya Septemba 2005 nchi sita za mazungumzo haya zilikubaliana Korea Kazkazini iachane na mradi wa kinyuklia na ipewe msaada, ufadhili wa nishati na kuhakikishiwa usalama. Makubaliano haya lakini yalisitishwa miezi miwili baada ya hapo kutokana na Korea Kaskazini kupinga vikwazo ilivyowekewa na Marekani kwa sababu ya tuhuma ya kuzifanyia biashara fedha zilizopatikana kwa njia haramu na pia kuchapisha fedha za bandia – vitendo ambavyo havikuhusiana na mradi wa kinyuklia.

Licha ya vikwazo hivi bado kuwepo, mjumbe Hill wa Marekani alisema ana matumaini mazuri kuhusu mkutano huu wa Beijing, baada ya kufanikiwa katika mazungumzo kati yake na mwakilishi wa Korea Kaskazini Kim Kye-Gwan yaliyofanyika mjini Berlin, Ujerumani mwezi uliopita. Bw. Hill wa Marekani alikanusha lakini ripoti iliyochapishwa na gazeti la Japan juu ya kusainiwa makubaliano kati ya Korea Kaskazini na Marekani kwenye mkutano uliopita mjini Berlin.

Nchi niyingine zinazoshiriki kwenye mkutano huu pamoja na Korea Kaskazini na Marekani ni Uchina, Korea Kusini, Urusi na Japan. Kabla ya mazungumzo kuanza, mjumbe wa Korea Kusini, Bw. Chun Yung Woo, alisema hadi sasa yamefanyika mazungumzo tu juu ya kuukomesha mradi wa kinyuklia wa Korea Kaskazini, lakini sasa ni wakati wa kuchukua hatua.