1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kuhusu nyuklia ya Iran yaporomoka

Admin.WagnerD24 Januari 2011

Baada ya kushindwa kuafikiana, sasa wawakilishi wa mataifa matano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Ujerumani wamesitisha mazungumzo yao na Iran kuhusu mradi wa kinyuklia wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/102EW
Ujumbe wa mazungumzo yaliyofeli
Ujumbe wa mazungumzo yaliyofeliPicha: FARS

Hata kabla ya mazungumzo hayo ya siku mbili yaliyoanza ijumaa iliyopita mjini Istanbul nchini Uturuki kumalizika, uvumi ulianza kuenea kwamba hakuna makubaliano yatakayofikiwa.

"Suala la mradi wa kinuklea wa Iran haliwezi kufumbuliwa katika duru moja au mbili za mazungumzo." Amesema Naibu Waziri wa Mambo ya nchi za Nje wa China, Wu Hailong katika taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa wizara hiyo, siku ya pili baada ya kushindwa mazungumzo ya Istanbul kati ya Tehran na madola matano yenye kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Ujerumani.

Ingawa China inaunga mkono maazimio ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa yanayoitaka Iran isitishe shughuli zake zinazobishwa za kinuklea,hata hivyo Beijing inaendeleza ushirikiano wa dhati wa nishati na biashara pamoja na Iran na imepinga pia vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya na Marekani dhidi ya Iran.

Umoja wa Ulaya wavunjika moyo

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton na mwakilishi wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia Saeid Jalili
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton na mwakilishi wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia Saeid JaliliPicha: picture-alliance/dpa/DW-Fotomontage

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Bibi Catherine Ashton amesema kwamba, Ulaya imevunjwa moyo sana na kuvunjika kwa mazungumzo haya.

"Haya sio matokeo tuliyokuwa tukitarajia. Tulitegemea majadiliano ambayo yangetufanya tusonge mbele. Na ndio maana tulijaandaa vya kutosha kuifikia shabaha hiyo. Nimevunjika moyo kuona kwamba jambo hilo halikuwezekana." Amesema Ashton.

Pande hizo mbili zilizokutana kwa mara ya kwanza mapema mwezi Disemba mwaka jana baada ya mazungumzo hayo kukwama kwa miezi 14, ziliagana jumamosi iliyopita mjini Istanbul bila ya kusema lini mazungumzo hayo yataendelea tena.

Hata hivyo, Rais Mahmoud Ahmadinedjad, akiwa ziarani kaskazini magharibi ya nchi hiyo amezungumzia "uwezekano wa kuanza duru mpya ya mazungumzo ya kinuklea yatakayoleta tija."

"Licha ya kushindwa duru hii ya mazungumzo,bado kuna nafasi ya kufikia makubaliano yatakayoridhisha pande zote, katika mazungumzo ya siku za mbele ikiwa upande wa pili utazingatia haki na hishma ya Iran." Amesema rais huyo wa Iran.

Mahmoud Ahmadinedjad anahoji hawakusema kama kadhia ya mradi wa kinuklea wa nchi yake inaweza kupatiwa ufumbuzi baada ya duru chache tu za mazungumzo.

"Ninaamini, baada ya duru mbili tatu za mazungumzo, mambo muhimu yamezungumzwa. Pande hizi mbili zinatambua kila upande unataka nini," ameongeza Ahmadinedjad.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mpitiaji: Grace Patricia Kabogo