Mengine ni mabishano juu ya Hifadhi ya ukimbizi.
16 Novemba 2017Kwa karibu mwezi mmoja sasa, Chama cha Christian Democratic Union-CDU na chama ndugu cha Bavaria Christian Social Union-CSU, pamoja na Free Democratic party-FDP kinachopendelea wafanyabiashara na chama cha Kijana, vimekuwa katika majadiliano makali katika kujaribu kuweka msingi wa kuundwa serikali ya kwanza ya kile kinachoitwa muungano wa Jamaica, jina linalotokana na rangi za vyama hivyo kufanana na bendera ya Jamaica.
Kila mahali wajerumani wengi wanazungumzia kuwa wakati umewadia wa taifa hili linaloongoza kiuchumi barani Ulaya kuwa na serikali inayofanya kazi, kwani kufuatia matokeo ya uchaguzi wa Septemba 24 kujulikana, hivi karibuni hata Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alielezea hisia zake juu ya uwezekano wa kuwepo na mkwamo wa kisiasa.
Alisema "hatutotenda haki ikiwa kila hatua inayochelewa tunachukulia kuwa ni kushindwa." Akawataka raia watulie na wawe na uvumilivu. Uvumilifu huo leo umo kwenye mtihani.
Ni siku ya mwisho ya mazungumzo ya awali ambayo ni maandalizi ya mazungumzo rasmi, yakitarajiwa kuendelaea hadi alfajiri ya kesho Ijumaa, ili kuyatatua masuala kadhaa ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi kwenye meza ya mazungumzo.
Suala la kwanza la mabishano ni Hifadhi ya ukimbizi, uhamiaji na kujumuika kwa familia
Baada ya majadiliano makali, CDU na CSU wamekubaliana kwamba serikali mpya isiruhusu zaidi ya wahamiaji wapya 200.000 kuingia Ujerumani kila mwaka kwa sababu za kibinadamu. FDP imependekeza wawe kati ya 150.000 na 250.000 kwa mwaka.
Chama cha Kijani kimetoa wito wale wakimbizi wenye kinga maalumu waruhusiwe kuzileta familia zao Ujerumani mara moja baada ya kuwasili. Chama hicho kinadai hatua kama hiyo itapunguza biashara ya binaadamu.
Suala la pili la mjadala ,ulinzi wa mazingira
Chama cha Kijani kinadai kiasi ya tani 90 milioni hadi 120 milioni za utoaji wa hewa chafu ya kaboni lazima kipunguzwe ili kufikia malengo ya hifadhi ya mazingira ya Ujerumani ifikapo mwaka 2020. CDU,CSU na FDP kwa upande wao wanasema kiwango kiwe cha chini zaidi, kati ya tani milioni 32 na milioni 66.
Suala la tatu ni Umoja wa Ulaya na sera ya sarafu katika kanda ya Euro
Mabishano ni juu ya kurekebisha sera ya Ujerumani kuelekea Ulaya. Jee iendelee kupigania kutanuliwa kwa kanda ya matumizi ya sarafu ya Euro, hata kama ina maana kutanuliwa mno kwa jukumu la pamoja la uokozi panapozuka matatizo? Upande huo FDP kinapinga hatua ya kuwaokoa wale waliojisababishia matatizo ya kifedha kama ilivyokuwa kwa Ugiriki.
Pia kinaupinga wito wa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wa kuwa na bajeti ya pamoja ya nchi za kanda ya euro. Kinyume chake chama cha Kijani kinayaunga mkono mapendekezo ya mageuzi ya Macron kuhusiana na kanda ya Euro na pia Umoja wa Ulaya.
Waraka wa pamoja kuhusu mjadala wa kuunda serikali ya muungano unatarajiwa kutolewa kesho Ijumaa. Muda wa kufikia maridhiano unakwenda mbio na swali ni jee baada ya siku 29 za majadiliano , maridhiano yatakuwa yamepatikana?
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahaman/ Richard Fuchs (DW)
Mhariri:Josephat Charo