Mazungumzo juu ya mpango wa nyuklia wa Iran yaanza.
15 Oktoba 2013Mataifa hayo sita yenye nguvu duniani Marekani, Urusi, China, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani yataiwekea msukumo mkali Iran katika mazungumzo ya siku mbili yanayofanyika mjini Geneva.
Mataifa hayo yanataka kuishawishi Iran kukubali kuachana na mpango wa nyuklia ili waweze kundolewa vikwazo vya uchumi walivyoekewa.
"Mazungumzo yameanza," alisema mmoja wa wanadiplomasia wa nchi za Magharibi.
Awali Iran imekuwa ikikataa kushiriki katika mazungumzo hayo na ikipuuzilia mbali shutuma za Magharibi kwamba wanapanga kutengeneza silaha za nyuklia.
Lakini tangu kuchaguliwa kwa rais mpya wa Iran Hassan Rouhani mwezi Juni mwaka huu kumekuwa na matumaini makubwa kuwa huenda kukawa na maafikiano hasa ikizingatiwa kuwa vikwazo ilivyoekewa Iran vinazidi kuyumbisha uchumi wa nchi hiyo.
Hata hivyo kuhusiana na suala zima la utengenezaji wa silaha za nyuklia Iran inaendelea kukanusha hilo huku ikisema kwamba mpango wake ni kwaajili ya matumizi ya amani.
Iran yasema iko tayari kushiriki kikamilifu katika mazungumzo
Kulingana na maafisa wa Iran, wako tayari kuridhia matakwa ya kimataifa ya kupunguza shughuli zao za nyuklia ili kujenga uaminifu kati yao na mataifa ya Magharibi.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Javad Zarif na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton ni miongoni mwa wanaohudhuria mazungumzo hayo.
Ashton amesema kwa sasa Iran imetoa mpango mpya wa kutatua hali ya wasiwasi kati yake na mataifa ya Magharibi. Naye Msemaji wa Umoja wa Ulaya Michael Mann hakutoa maelezo zaidi juu ya mpango huo lakini akasema ujumbe ulioandamana na Ashton utaliangazia jambo hilo kwa kina.
Huku hayo yakiarifiwa Israel imesema mataifa hayo sita yanayoendelea na mazungumzo na Iran yanapaswa kuhakikisha kuwa Iran inaachana kabisa na mpango wake wa nyuklia na kutoiondolea vikwazo .
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema mtambo wa kutengenezea nyuklia wa iran unapaswa kufungwa na zana vyote ziliomo ndani kusafirishwa hadi mataifa ya ulaya.
Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman