Mazungumzo baina ya Rais Mbeki na Rais Mugabe nchini Zimbabwe yamalizika.
9 Mei 2008Hata hivyo mazungumzo hayo yamemalizika pasipokutolewa kwa taarifa yoyote juu ya nini walichokijadili katika mazungumzo hayo.
Wakati huo huo mabalozi wa nchi za kigeni wamewatembelea waathirika walioshambuliwa na wapiganaji wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa rais Mugabe.
Rais Mbeki amekuwa na mazungumzo mazito na rais Robert Mugabe juu ya hali ya mgogoro katika Uchaguzi wa mwezi machi.
Mbeki ambaye ni mpatanishi mkubwa, baada ya kuwasili mjini Harare alikwenda moja kwa moja kwa ajili ya mazungumzo na rais Mugabe ikiwa ni ziara yake kwanza nchini humo tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais.
Mazungumzo hayo ambayo yamefanyika katika Ikulu ya nchi hiyo yamechukua muda wa masaa matatu kabla ya Mbeki hajaelekea kwenye ubalozi wa Afrika Kusini mjini harare pasipo kutoa taarifa yoyote kwa waandishi wa habari juu ya mazungumzo yao.
Chama cha Upinzani cha MDC, ambacho kilishinda uwakilishi mwingi Bungeni na ambacho kiongozi wake alimshinda rais Mugabe katika awamu ya kwanza ya Uchaguzi Machi 29,kilitaka Bw Mbeki avuliwe wadhifa wake kama mpatanishi wa mgogoro huo kutokana na kushindwa kumwambia ukweli rais Mugabe.
Juhudi hizi mpya za upatanishi zinakuja huku kukiwa na madai ya kuendelea kwa ghasia nchini humo ambazo zinalaumiwa kufanywa na magenge ya mgambo yanayounga mkono serikali ya Mugabe.
Kiongozi wa chama Kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change -MDC, Morgan Tsvangirai amabaye Rais Mbeki nimpatanishi wake na Rais Mugabe, amesema hajakaribishwa katika mazungumzo yeyote na Rais huyo wa Afrika Kusini.
Msemaji wa chama hicho, George Simbotshiwe, amesema wanatambua kuwa kiongozi huyo yuko Zimabwe na anakutana na Rais Mugabe lakini kama Chama hawana mawasiliano yoyote ya kiofisi kuwa atakutana na chama cha MDC au kiongozi wake.
Bwana Tsvangirai, amekuwa nje ya Zimababwe kwa kipindi cha wiki kadhaa sasa, akikutana na viongozi wa Afrika na mabalozi ikiwa ni juhudi za kutaka kuongezwa nguvu ya kumshawishi Rais Robert Mugabe kuachia madaraka baada ya miaka ishirini na nane kumalizika akiwa madarakani.
Viongozi kutokaka mataifa kumi na nne wanachama wa SADC, mwezi uliopita walikutana mjini Lusaka Zambia,na walimtaka rais Mbeki aendelee na kazi yake ya upatanishi baina ya Chama Tawala cha ZANU-PF kinachoongozwa na rais Mugabe pamoja na chama cha MDC.
Rais Mbeki amekuwa akikata kumpinga rais Mugabe hadharani, mbali na kwamba nchi yake imejikuta ikiingia katika gharama mbalimbali za kiuchumi, huku kiasi cha raia wa Zimbabwe milioni tatu wakiaminika kuwa wanatafuta kazi nchini Afrika Kusini.
Wakati huo huo, Mabalozi kutoka Marekani, Umoja wa Ulaya, Ujerumani, Sweden na Angola walioko mjini Harare, wamewatembelea waathirika wa machafuko hayo ya kisiasa walioko kaztika Kliniki ya Avenues mjini Harare.
Kwa upande mwingine Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Zimbabwe amesema kuwa madai yote ya matokeo ya Bunge ya uchaguzi wa mwezi Machi, yaliyopelekwa mahakamani hapo yatashughulikiwa katika kipindi cha miezi sita.
Aidha wakati rais Mbeki amekutana na Rais Mugabe, Chama cha madaktari wanaotetea haki za binadamu nchini humo kimesema kuwa Vurugu na manyanaso zinazodaiwa kufanywa na makundi ya Rais Mugabe zimezidi kuendelea kila siku.
Taarifa iliyotolewa na chama hicho cha madaktari imesema kuwa mpaka sasa chama hicho kimepokea taarifa za watu mia tisa waliofanyiwa manyanyaso ya aina mbalimbali lakini kikabainisha kuwa idadi hiyo ni makadilio tu lakini vurugu kwa sasa zimefikia kiwango kibaya zaidi.
Mpaka sasa chama cha Upinzani kinadai kuwa wafuasi wake wapatao thelethini wameshauawa katika mashambulio yanayofanywa na wafuasi wa rais Mugabe na tangu uchaguzi ufanyike maelfu ya watu wameshakumbwa na mateso mbalimbali.