1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazingira yanapochangaya siasa na uchumi

Helle Jeppesen26 Novemba 2010

Mwangwi wa kufeli kwa mkutano wa Tabia Nchi wa Copenhagen ulihanikiza Ulaya nzima na sasa mkutano kama huo unafanyika mjini Cancun na tena patakuwa na mabishano baina ya siasa, uchumi na hatima ya sayari ya dunia.

https://p.dw.com/p/QItG
Kampeni za kutetea ulinzi wa mazingira
Kampeni za kutetea ulinzi wa mazingiraPicha: picture alliance/dpa

Mkurugenzi wa Nishati na Siasa za Tabia Nchi kwenye Kampuni ya Ushauri ya Ecofys ya mjini Cologne, Niklas Höhne, hatarajii maajabu yoyote makubwa kwa mkutano huu wa Cancun. Anasema kuwa matatizo ambayo yalifeli kupatiwa ufumbuzi kwenye mkutano wa Copenhagen hayatokani na dunia, bali ni ukosefu wa utashi wa kisiasa.

Höhne anayaona maendeleo ya kisiasa tangu kumalizika kwa mkutano wa Copenhagen kama yanazidi kuudhi, na ndio maana haiwezekani kwa Umoja wa Ulaya kufikia lengo la kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kutoka asilimia 20 hadi 30 hapo ifikapo mwaka 2020.

Ujerumani imejiwekea lengo lake yenyewe kwamba hadi kufikia mwaka 2020 iwe imepunguza uzalishaji wa hewa chafu kwa asilimia 40 ikilinganishwa na mwaka 1990. Kufanikisha hilo, ndipo serikali ya Shirikisho ikarefusha matumizi ya vinu vyake vya atomiki, ili ipate kodi inayotokana na nishati hiyo kusaidia kutimiza lengo la upunguzaji. Jambo hili linaonekana kuwa ni kinyume-mbele na wachambuzi wa siasa za tabia nchi na nishati.

Kwanza, urefushaji huu wa muda kwa maslahi ya kuzalisha umeme, ambao nao utazalisha faida ya fedha zitakazotumika kufidia uchafuzi wa mazingira ni kinyume cha mambo. Maana unapokuwa unategemea fedha za uharibifu kwa utengezaji, maana yake ni kwamba unahalalisha uharibifu. Na hili si jambo la kiuchumi hata kidogo. Pili, ni kuwa jambo hili linakwaza jitihada za kutumia nishati jadidifu katika teknolojia mpya, maana umeme unaozalishwa na nishati hizo unajikuta una ushindani mkubwa kwenye soko.

Lakini katikati ya siasa hizi za nishati na mazingira, bado kuna fursa ya uchumi kuja juu na maendeleo kupatikana. Ndivyo anavyoamini Catharina Beyer wa Ecofys, ambaye anasema kuwa kuna uhusiano baina ya nishati na masoko. Mtu anaweza kuyatumia mambo haya kwa ubunifu, kwa mfano, kwa kuandika juu ya maudhui haya na halafu akauza wazo kwa wanaohusika na kutengeneza faida kubwa.

Kwa mfano, ni kampuni ya vifaa vya elektroniki ya Siemens, ambayo imevunja rekodi kwa namna inavyoshughulikia masuala ya kiteknolojia chini ya dhana yake mpya ya tekonoljia ya kijani, lengo likiwa ni kuoanisha teknolojia ya utengenezaji vifaa na teknolojia ya utunzaji wa mazingira.

Na hapa ndipo unapokuja umuhimu wa teknolojia kwa maisha ya mwanaadamu, kwamba sio tu kwamba kampuni inapotumia njia kama hii, hutumia nishati kwa ufanisi zaidi na hivyo kuzalisha kiwango kidogo cha hewa chafu, bali pia huyasaidia mazingira na hivyo viumbe wanaoishi kwenye sayari hii.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Zhang Danhong

Mhariri: Othman Miraji