1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

May bado akabiliwa na kishindo cha Brexit

19 Novemba 2018

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May anatarajiwa kutetea pendekezo lake la Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, kwa wafanyabiashara huku majadiliano magumu yakitarajiwa katika mkutano wa Umoja wa Ulaya, Brussels.

https://p.dw.com/p/38Uif
England | PK Theresa May
Picha: Reuters/Pool/I. Vogler

Waziri Mkuu Theresa May ataayaambia mashirika ya wafanyabiashara wa viwanda nchini Uingereza kwamba anaamini atafikia makubaliano na baraza la Ulaya  kuelekea mkutano wa Kilele siku ya Jumapili utakaopelekea kutiwa saini makubaliano ya Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya.

Katika mkutano wake na kundi hilo la washawishi wa kibiashara May atazungumzia masuala tete  na muhimu kwa Uingereza kama udhibiti wa mipaka, fedha na sheria.

Theresa May
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May Picha: picture-alliance/empics

Akizungumzia suala la uhamiaji ambalo ndilo jambo linalowasumbua vichwa wafanyabiashara wengi wanaoona watakosa watu walio na ujuzi, May ataahidi kuanzisha mikakati thabiti itakayowavutia wahamiaji walio na ujuzi zaidi duniani.

May amesema anaamini anaweza kufanikiwa katika makubaliano yake na Baraza la Ulaya ambapo baadaye makubaliano hayo yatapelekwa bungeni ili kujadiliwa na kupitishwa iwapo kila mwanachama ataridhia.

Waziri huyo Mkuu wa Uingereza Theresa May ambaye baraza lake la mawaziri  lilipitisha mapendekezo yake ya kuondoka Umoja wa Ulaya wiki iliopita bado anakabiliwa na changamoto ya maamuzi yake kupitishwa na bunge ambalo baadhi ya wanachama wake hawana Imani nae.

Hata hivyo May amekubali kuwa mchakato wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit ni mgumu na utaendelea kuwa mgumu hadi wakati wakatakapofikia makubaliano lakini akasema kile anachokifanya ni kwa manufaa ya taifa na waingereza wenyewe.

Wabunge waasi wajaribu kuwasilisha kura ya kutokuwa na Imani na Waziri Mkuu May

Majadiliano ya Brussels yanatarajiwa kufunga mkataba wa kisiasa utakaotoa muelekeo wa ushirikiano wa Umoja wa Ulaya na Uingereza baada ya taifa hilo kujitoa katika Umoja huo.

Großbritannien - Theresa May im House of Commons
Waziri Mkuu Theresa May akiwa bungeni UingerezaPicha: picture-alliance/empics

Pamoja na hayo Waziri mkuu May anakabiliwa na kishindo kikubwa nyumbani baada ya wabunge waasi wakijaribu kupitisha kura ya kutokuwa na Imani nae kufuatia mpango wake wa Brexit.

Mbunge Simon Clarke akizungumza na shirika la habari la BBC, amesema leo ndio siku ambayo hatua zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya May. Clarke ameshawasilisha barua ya kutokuwa na Imani na waziri mkuu huku akisema kila saa na kila siku ambapo mpango wa Brexit unakataliwa ni siku inayopotezwa ya kuwa na majadiliano ya kuaminika.

Hii leo Mawaziri wa nchi 27 wanaounda Umoja wa Ulaya wanakutana kujadili suala la Brexit kabla ya mkutano wa kilele wa viongozi utakaofanyika siku ya Jumapili hii mjini Brussels.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu