Mawaziri, wakuu wa nchi wawasili Doha
5 Desemba 2012Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon anatarajiwa kuhutubia mkutano huo wa washiriki zaidi ya 11,000 majira ya saa 9 kwa saa za Afrika mashariki, na anatarajiwa kuhimiza mataifa kuweka pembeni tofauti zao kwa ajili ya mustakabali ya sayari ya dunia.
Hata baada ya kutolewa kwa tahadhari juu ya hatari inayoikabili dunia kutokana na gesi chagu, wangalizi wanasema karibu mataifa 200 yanayoshiriki mazungumzo ya Doha yemeendelea kugawanyika juu ya masuala muhimu kwa ajili ya kufukia makubaliano kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Mataifa maskini yanasisitiza kuwa mataifa ya magharibi yakubali kupunguza kwa haraka na kwa kiwango kikubwa, utoaji wa gesi chafu na yajifunge kuchangia mfuko wa mazingira kuanzia mwaka 2013 kusaidia mataifa kukabiliana na hali ya ukame inayozidi kuwa mbaya, mafuriko, vimbunga na kufura kwa bahari.
Shabaha ya Umoja wa Mataifa
Maazimio kuhusu masuali yote mawili kabla ya kumalizika kwa mkutano huo siku ya Ijumaa yatasafisha njia ya kuwepo na mkataba mpya na mpana ambao unatakiwa usainiwe kabla ya mwaka 2015 na kuanzwa kutekelezwa mwaka 2020 ili kupunguza joto la dunia.
Shabaha ya Umoja wa Mataifa ni kupunguza kiwango cha joto la dunia kufikia nyuzi joto mbili, ambazo wanasayansi wanasema zinaweza kusisadia dunia kuepekua athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabia nchi.
Mkuu wa Tabia Nchi wa Umoja wa Mataifa, Christiana Figueres, ameelezea kusikitishwa kwake siku ya Jumatatu, kuhusiana na kasi ndogo ya mazungumzo hayo, wakati baadi ya wajumbe wakionyesha hofu ya mkwamo kabla ya kuwasili kwa mawaziri kutoa msukumo wa mwisho wa kisiasa.
Wakuu wa serikali kutoa msukumo wa kisiasa
Wakuu watano wa nchi na serikali wanatarajiwa kuhutubia mkutano wa leo - kutoka Gabon, Mauritania, Samoa, Ethiopia na Swaziland. Mazungumzom ya Doha yanalenga kukamilisha awamu ya pili ya mkataba wa Kyoto, mkataba pekee unaoileta pamoja dunia kuhusu kupunguza utoaji wa gesi chafu, lakini wajumbe wanatofautiana juu ya muda wake na shabaha za mataifa.
Duru ya kwanza ya mkatabaka huo inazitaka nchi karibu 40 tajiri zaidi na Umoja wa Ulaya, kupunguza uotaji wa gesi, lakini inaziacha pembeni nchi mbili zinazoongoza kwa utoaji wa gesi chafu - Marekani ambayo ilikataa kusaini mkataba huo, na China ambayo iliachwa kwa sababu ni nchi inayoendelea.
Eneo linigine linalosababisha mfarakano ni fedha. Nchi zilizoendelea zinatakiwa kuonyesha namna zinavyopanga kutimiza ahadi za kuchangia dola za Marekani bilioni 100 - kiasi kilichoongezeka kutoka dola bilioni 30 kati ya mwaka 2010 na 2012, kwa ajila ya mpango wa fidia ya tabia nchi kwa mataifa maskini kila mwaka kufukifia mwaka 2020. Mataifa yanaoendelea yanasema yanahitaji jumla ya dola bilioni 60 kuanzia sasa hadi 2015, lakini mpaka sasa hakuna ahadi yoyote iliyotolewa.
Ni hali ya kutia wasi wasi
Ripoti ya utafiti iliyotolewa siku ya Jumapili imeonya kuwa dunia inaweza kuwa inaelekea juu ya kiwango cha nyuzi joto 5 kufikia mwaka 2100 -- kiwango ambacho ni mara mbili ya kikomo cha nyuzi 2 ambacho Umoja wa Mataifa unalenga kukifikia.
Na ripoti ya uchumi iliyotolewa leo Jumanne imesema hata shabaha ya uchafuzi wa mazingira wa kiwango cha asilimia 0 kwa mataifa yaliyoendelea kufikia mwaka 2030 haitasitisha mabadiliko mabaya ya tabianchi, na mataifa maskini pia yanapaswa kutekeleza wajibu wao.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Mohammed Khelef