Mawaziri wa zamani wa jimbo la Catalonia wawekwa kizuizini
3 Novemba 2017Mawaziri hao wa zamani wa Catalonia wanasubiri uchunguzi ukamilike kuhusu kushiriki kwao katika harakati za kutaka uhuru wa jimbo lao. Paul Bekaert, wakili wa aliyekuwa Rais wa Catalonia Carles Puigdemont, alimeliambia shirika la Televisheni la nchini Ubelgiji VRT kwamba mteja wake ambaye kwa sasa yuko nchini Ubelgiji ameapa kuwa atapinga hatua ya kurudishwa nchini Uhispania.
Wakili Bekaert amefafanua kwamba kutolewa kwa waranti huo kwa bwana Puigdemont na mawaziri wengine wanne wa jimbo la Catalonia ambao wapo pamoja naye nchini Ubelgiji kutaiwezesha mahakama ya Uhispania kutoa maombi kwa waendesha mashtaka wa nchini Ubelgiji ili kumrudisha Puigdemont nchini Uhispania. Wakili wa Puigdemont amesema waranti huo utawezesha mteja wake kukamatwa mahala popote pale barani Ulaya.
Wanasiasa hao watano walitakiwa kufika mahakamani katika mji wa Madrid kujibu mashtaka ya uasi, uchochezi na matumizi mabaya ya fedha za umma makosa ambayo kifungo chake kinafika hadi miaka 30 jela. Mahakama ya nchini Uhispania tayari imeamuru kuwekwa kizuizini bila ya kupewa dhamana kwa viongozi wa seriakli ya zamani wapatao wanane waliofikishwa mbele ya mahakama hapo jana Alhamisi. Watuhumiwa hao ni pamoja na aliyekuwa makamu wa rais wa jimbo la Catalonia Oriol Junqueras. Mtuhumiwa wa tisa aliyekuwa pia mjumbe wa serikali hiyo ya Catalonia alipewa dhamana ya Euro elfu 50. Katika ujumbe uliorekodiwa na kutangazwa kwenye kituo kimoja cha televisheni cha Catalonia Puigdemont ameitaka serikali iwaachie wajumbe wake wote wanane.
Kiongozi huyo aliyenyang'anywa madaraka na seriklali kuu ya Uhispania amesema kuwekwa kizuizini kwa aliyekuwa makamu wake wa rais na baraza lake la mawaziri ni kitendo kinachokiuka kanuni na misingi ya kidemokrasia. Puigdemont amesisitiza kuwa hatorejea Uhispania mpaka atakapohakikishiwa kuwa atatendewa haki atakapofikishwa mahakamani.
Carles Puigdemont na mawaziri wake wa zamani wa afya,wa kilimo, wa elimu,na wa utamaduni, wanaweza kukamatwa mara moja na mamlaka ya Ubelgiji iwapo waendesha mashtaka wataidhinisha nyaraka zote ziliyowasilishwa, kama hakutokuwepo vikwazo vya kisheria, basi Puigdemont na wenzake wanaweza kusafirishwa ndani ya siku chache. Ubelgiji hata hivyo ina siku hadi 60 kabla ya kuamua kuwapeleka watuhumiwa hao nchini Uhispania.
Hayo yakiarifiwa, mamia ya watu wamejitokeza kufanya maandamano katika barabara za mjini Barcelona kupinga kuwekwa kizuizini wajumbe wa bunge la Catalonia. Umoja wa Ulaya unamuunga mkono waziri mkuu Mariano Rajoy. Nicola Sturgeon kiongozi wa Scotland ambayo ni sehemu ya Uingereza iliyo na ndoto ya kujitenga na nchi hiyo, amelaani kuwekwa kizuizini kwa mawaziri wa zamani wa Catalonia.
Benki kuu ya Uhispania imeonya kwamba hali ya uchumi wa nchi hiyo inaweza kuzorota iwapo mgogoro wa jimbo la Catalonia utaendelea. Kuna dalili za kuongezeka kwa mgawanyiko katika kambi inayotaka kujitenga,kutokana na wengi kuwa hawafurahii hatua ya Puigdemont, hasa kwa wakati huu ambapo yuko mbali na eneo ambalo anatarajiwa kuongoza uhuru wake.
Mwandishi:Zainab Aziz/FPAE/DPAE/APE
Mhariri: Gakuba, Daniel