Mawaziri wa Umoja wa Ulaya wazungumzia mzozo wa wakimbizi
18 Julai 2017Umoja wa Ulaya unasimamiwa opereshini mbili baharini zikiwemo dazeni kadhaa ya meli katika eneo la bahari kati ya Italia na Libya. Lakini opereshini zote hizo zlizopewa majina;"Triton" na "Sophia" hazikuyafikia malengo yaliyowekwa. Opereshini Triton imelengwa kuwaokoa wakimbizi wanaokabiliwa na hatari ya kuzama kati ya Sicilia na Lampedusa. Sophia ni opereshini iliyolegwa kupambana na makundi ya wahalifu wanaosafirisha watu kinyume na sheria. Hata hivyo na licha ya juhudi za kila aina, idadi ya wakimbizi wanaozama inazidi kuongezeka. Mnamo nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2017 idadi yao ilipindukia watu 2000 - idadi halisi lakini haijulikani. Licha ya juhudi za kuimarisha shughuli za walinzi wa fukwe na bahari nchini Libya na kushirikisha opereshini Sophia katika juhudi hizo, idadi ya wanaosafirishwa kinyume na sheria inaendelea kuongezeka.
Mnamo nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2017 walifikia watu 86.000 wengi wao wakiwa wahamiaji kutoka Afrika au watu wanaoomba kinga ya ukimbizi katika bandari za Italia.
Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa ulaya walikutana mjini Brussels na kutathmini yaliyotokana na opereshini hizo pamoja na kusaka njia za kuziimarisha.
Mashirika yasiyomilikiwa na serikali yanakanusha tuhuma za Italia
Italia wanakofikia wengi wa wahamiaji hao, inashinikiza na inatishia kutotia saini makubaliano ya kurefusha shughuli za Opereshini Sophia. Muda wa makubaliano hayo unamalizika Julai 27 inayokuja. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Italia Angelino Alfano anavuta wakati anasema mada hiyo kwa sasa haijaorodheshwa katika ajenda ya mazungumzo na kwamba itashughulikiwa wakati wa kurefushwa makubaliano hayo utakapowadia.
Italia inayatuhumu mashirika yasiyomilikiwa na serikali kushirikiana na makundi hayo ya wahalifu. Katika mahojiano na DW, shirika la SOS Mediterenia limekanusha moja kwa moja tuhuma hizo.
Watu wanazidi kufa licha ya juhudi za uokozi kuimarishwa
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Austria Sebastian Kurz anasema: "Kile tunachobidi kufanya ni kuhakikisha watu hawavutiwi kabisa na fikra ya kuelekea Libya. Na hilo linawezekana tu tutakapozifunga njia zote katika bahari ya Mediterenia. Kila wakati ambapo watu wengi wataelekea Libya ndipo nao watu wengi watakapojikuta wakisafirishwa na makundi ya wahalifu katika hali ngumu kupita kiasi na ndipo nayo pia idadi ya wanaoyatia hatarini maisha yao katika bahari ya Mediterenia itakapozidi kuongezeka."
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Austria ameelezea masikitio yake kuona kwamba idadi kubwa zaidi ya watu wanaendelea kupoteza maisha yao licha ya kwamba Umoja wa ulaya unaendelea kuwekeza katika shughuli za uokozi.
Mwandishi: Bernd Riegert/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Mohammed Khelef