Mawaziri wa Ulaya wazijadili Urusi na Burundi
14 Desemba 2015Hayo yameelezwa leo na Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini wakati wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Ulaya mjini Brussels. Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano huo, Mogherini amesema anaelewa hilo litajadiliwa katika mkutano wa Baraza la Ulaya baadae wiki hii kama ambavyo imekuwa siku zote pale linapokuja suala la vikwazo vya Urusi.
Amesema haoni matatizo makubwa kutoka kwa nchi yeyote mwanachama kuhusu maamuzi ya kisiasa katika kurefusha vikwazo hivyo. Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Paolo Gentiloni amesema hatabiri mazungumzo marefu kuhusu vikwazo katika mkutano huo wa kilele.
Italia moja kati ya washirika mkuu wa kibiashara wa Urusi barani Ulaya, ilitoa wito wa kufanyika mazungumzo hayo wakati ambapo viongozi wa mataifa 28 ya Umoja wa Ulaya watakapokutana siku za Alhamisi na Ijumaa, ikimaanisha kwamba suala la kurefushwa vikwazo halikujadiliwa kama ilivyopangwa katika mkutano wa mabalozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, wiki iliyopita. Italia inataka njia ya mawasiliano na Urusi iwe wazi, licha ya mzozo wa Ukraine.
Wataka machafuko yakomeshwe Burundi
Wakati huo huo, mawaziri hao leo wametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kukomesha machafuko yanayoendelea Burundi, baada ya watu kadhaa kuripotiwa kuuawa katika siku za hivi karibuni. Mogherini amesema katika muda huu wanafanya kazi kuhakikisha wanasaidia kukomesha machafuko yanayoendelea nchini Burundi. Amesema ni muhimu mazungumzo kuhusu Burundi yakaanza haraka.
''Tunawasiliana na uongozi wa Umoja wa Afrika ili kuwezesha mazungumzo yatakayoongozwa na umoja huo. Na pia tumejiandaa kutoa msaada wa kifedha kusaidia kuyawezesha mazungumzo hayo ili yaanze haraka, kwa sababu lazima tukomeshe machafuko,'' amesema Mogherini
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Didier Reynders amesema matukio ya hivi karibuni ni janga na kwamba ana matumaini pamoja na wenzake watafanikiwa kupeleka ujumbe kwa Umoja wa Afrika na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya pia utaizungumzia Libya, Iraq pamoja na juhudi za Uturuki kutaka kujiunga kwenye Umoja wa Ulaya, kwa kukubali kuanzisha mazungumzo ya masharti ya kifedha ya umoja huo, kama sehemu ya mkataba mkubwa wa kuisaidia Ulaya kuutatua mzozo wa wakimbizi.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE
Mhariri: Yusuf Saumu