1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Paris huenda yakaugubika mkutano huo

Admin.WagnerD19 Januari 2015

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana leo mjini Brussels, wakati mashambulizi mjini Paris na kugunduliwa kwa wapiganaji wa Jihadi nchini Ubeligiji, vikigonga vichwa vya habari.

https://p.dw.com/p/1EMVz
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini (Kushoto) akisalimiana na waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Uhispania, Jose Manuel Garcia-Margallo mjini Brussels
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini (Kushoto) akisalimiana na waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Uhispania, Jose Manuel Garcia-Margallo mjini BrusselsPicha: Reuters/Y. Herman

Mashambulizi ya Paris yaliofanywa na raia watatu wa Ufaransa waliokuwa na mafungamano na makundi kadhaa ya Jihadi nchini Syria na Yemen , pamoja na operesheni nchini Ubeligiji dhidi ya ugaidi, ni masuala yaliouandama Umoja wa ulaya, pakizingatiwa hasa juu ya haja ya ushirikiano kupambana na kitisho cha wapiganaji wa kigeni.

Mawaziri hao wa mambo ya nchi za nje hawatochukuwa uamuzi wowote, zaidi ya kuzingatia mlolongo wa hatua wakati Umoja huo ukijitayarisha kwa mkutano wa Viongozi wake wakuu mwezi ujao, utakaozungumzia mapambano dhidi ya ugaidi. Chini ya zingatio hilo Mawaziri hao wataitathimini mgogoro nchini Libya ambao umegeuka kuwa mbaya zaidi. Jumamosi iliopita, Umoja wa ulaya uliyapongeza makundi yanayopigana nchini Libya kwa kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya Umoja wa kitaifa, ingawa bado njia ni ndefu kuleta amani katika taifa hilo lililo ukingoni mwa kuporomoka.

Tafakari juu ya uhusiano kati ya Ulaya na Urusi

Lakini ajenda kuu ya mkutano wao wa leo, ni kutathmini uhusiano na Urusi, suala ambalo huenda likawa ni mtihani kwa Mkuu wa masuala ya kigeni wa Umoja huo Federica Mogherini. Mogherini alitawanya waraka wakujadiliwa na mkutano huo, ambapo amewataka mawaziri kuzingatia maeneo yanayoweza kusaidia kurejesha tena mafungamano na Urusi, kama vuile katika suala la Syria , Iraq na kitisho cha kundi la Dola la Kiislamu. Kubwa zaidi waraka wake unapendekeza paweko na tafauti baina ya vikwazo kuhusiana na hatua ya Urusi kulitwaa eneo la Crimea na vikwazo vinavyohusiana na hatua yake ya kuhusika kwake na mzozo wa mashariki mwa Ukraine.

Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye nchi yake inatuhumiwa kujiingiza katika mzozo wa Ukraine.
Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye nchi yake inatuhumiwa kujiingiza katika mzozo wa Ukraine.Picha: Getty Images/AFP/Y.Kadobnov

Umoja wa ulaya unajikita hasa katika kuhakikisha makubaliano ya amani ya Minsk yalioungwa mkono na Urusi mwezi Septemba, yanatekelezwa na yanalenga kumaliza mapigano mashariki ya Ukraine, ambayo yamesababisha karibu watu 4,800 kuuwawa. Hata hivyo kwa wakosoaji, zingatio hilo kama lilivyo katika waraka huo wa mjadala wa Bibi Mogherini, ni hatari, likikaribiana na kuikubali hatua ya Urusi kulitwaa eneo la Crimea mwezi Machi 2014, ambapo Rais Vladmir Putin amesisitiza kwamba kamwe hatubatilisha uamuzi wake.

Rais wa Umoja wa Ulaya Donald Tusk ameliweka suala la Urusi nafasi ya juu katika ajenda ya mkutano wa kiilele wa viongozi wa Umoja huo mwezi Machi, ambapo watapaswa kuamuwa nini cha kufanya,wakianzia na suala la kurefushwa kwa vikwazo dhidi ya Urusi.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman,

Mhariri: Josephat Charo