Mawaziri wa Ujerumani wakubali kuongeza msaada kuiokoa Euro
1 Septemba 2011Lakini si wote walioridhika na mageuzi yanayotazamiwa kufanywa katika mpango huo wa kuikoa sarafu ya Euro. Kwa hivyo, kuna hofu kuwa baadhi ya wanasiasa, katika serikali ya mseto ya Kansela Angela Merkel, huenda wakaupinga mpango huo utakapowasilishwa bungeni baadae mwezi huu.
Ikiwa wanasiasa hao katika serikali ya mseto ya kihafidhina watakataa kuyaunga mkono mageuzi hayo, basi Kansela Merkel hatokuwa na budi kwenda kwa vyama vya upinzani ili asaidiwe kuupitisha mpango huo bungeni. Lakini hapo kuna hatari ya kuitumbukiza serikali yake katika mzozo na hata kusababisha uchaguzi kuitishwa mapema.
Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble akiutetea mpango huo amesema, uamuzi uliopitishwa na baraza la mawaziri umedhihirisha nia thabiti ya serikali kuiimarisha sarafu ya Euro.
Kuambatana na mageuzi yanayopangwa kufanywa katika mpango wa EFSF, mchango wa Ujerumani katika mfuko huo wa fedha, utaongezeka hadi kufikia Euro bilioni 211 kutoka mchango wa zamani wa bilioni 123. Vile vile, madeni ya nchi za kanda ya Euro katika masoko ya fedha yatakusanywa kwa kununua hisa za serikali hizo zinazoshindwa kuwalipa wakopeshaji wake.
Wabunge kadhaa katika serikali ya Merkel wanazingatia kuupinga mpango huo wa Umoja wa Ulaya, kwani wapiga kura wa Ujerumani, wanapinga mpango utakaoifanya Ujerumani kutoa fedha zaidi ili kusaidia kudhibiti mzozo wa madeni. Katika Umoja wa Ulaya, Ujerumani ni mfadhili mkuu wa mpango huo wa msaada. Ili kuongeza uwezekano wa kuungwa mkono, serikali ya Merkel inatazamiwa kukubali kulipa bunge, haki ya kuwa na usemi katika maamuzi yanayohusika na malipo ya mfuko huo.
Lakini uchaguzi unafanywa katika majimbo ya mawili ya Ujerumani, kabla ya mpango wa uokozi EFSF kuwakilishwa bungeni. Ikiwa chama cha Merkel cha CDU hakitofanikiwa katika chaguzi hizo, basi hiyo huenda ikazusha hofu miongoni mwa wabunge wa Merkel. Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni yaliyotangazwa hapo jana, mara nyingine yameonyesha kuwa serikali ya mseto ya Merkel itatolewa madarakani kama uchaguzi utafanywa hivi sasa. Kwa mujibu wa uchunguzi huo, chama cha SPD na cha Kijani vinaongoza. Kwa hivyo, wachambuzi wanasema, katika hali kama hiyo, bila shaka serikali haitotaka kuitisha mapema uchaguzi.
Mwanadishi: Martin, Prema/dpae
Mhariri: Abdul-Rahman